Mara baada ya kusambaa kwa barua ya Twaweza iliyoandikwa kutokea Costech, Taasisi ya Twaweza imejibu kimya kimya barua waliyoandikiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Julai 11 2018.
Twaweza imechukua hatua hiyo baada ya kutakiwa na Costech kujieleza kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria kwa kosa la kutoa matokeo ya utafiti bila ruhusa.
Akizungumza na www.eatv.tv Meneja utetezi wa taasisi ya Twaweza Annastazia Rugaba amesema kuwa tayari Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze ameshajibu barua hiyo tangu Julai 13 na sasa wanasubiri majibu ya Costech.
Julai 11, mwaka huu Costech iliiandikia barua Twaweza na kuitaka kutoa maelezo hayo ikiwa ni siku chache baada ya kutoa ripoti ya utafiti uliopewa jina la ‘Sauti za Wananchi.’
Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuporomoka kwa ukaribu wa wananchi na vyama vya siasa, utekelezaji wa majukumu kwa viongozi walioko madarakani, Rais anavyotekeleza majukumu tangu alipoingia madarakani na uhuru wa kujieleza katika baadhi ya maeneo.