F Yanga wagomea safari | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Yanga wagomea safari


Licha ya kumalizana vizuri na mabosi wa Yanga juzi, tetesi zinadai kuwa hali ni tete kwa weachezaji wa Yanga kutokana na kuonekana kuugomea mpango wa kuweka kambi Morogoro ili kujiandaa na mchezo dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

Safari ya kuelekea Morogoro ambayo ilipaswa kufanyika jana ilikwama tena na badala yake programu ya kuendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi ikaendelea japo wachezaji baadhi wakigoma kwenda kushiriki mazoezi hayo.

Wachezaji ambao hawakufika mazoezini ni pamoja na  beki Hassan Kessy, kipa Beno Kakolanya, Andrew Vincent , Ibrahim Ajibu na Kelvin Yondani, ambaye alitegemewa kuhudhuria mazoezi hayo baada ya kukutana na Abbas Tarimba siku kadhaa zilizopita.

Haijajulikana kama safari hiyo itakuwepo tena au la kutokana na mgomo huo ambao wachezaji wamekuwa wakiuendeleza ambapo walipaswa kuondoka jana kuelekea Morogoro kwa ajili ya kambi maalum kujiwinda dhidi ya Gor Mahia FC katika mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa jijini Dar es Salaam, Julai 29 2018.

Katika kikao walichokaa juzi viongozi wa Yanga pamoja na wachezaji wa timu hiyo kilikuwa na lengo la kujadili juu ya mgomo baridi ambao umekuwa ukifanywa na wachezaji wakidai stahiki zao.

Yanga inakuwa katika hali ya sintofahamu baada ya kuandamwa na jinamizi la viongozi wake kujiuzulu akiwemo aliyekuwa katibu mkuu Boniface Mkwasa, Mwenyekiti wa kamati ya kuinusuru Yanga Abbas Tarimba, Makamu mwenyekiti Clement Sanga,  pamoja na wajumbe mbalimbali wa kamati ya utendaji ambao wameshachia ngazi.