F Kanisa Katoliki lamzika mtawa aliyejiua kwa heshima, wafunguka haya | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kanisa Katoliki lamzika mtawa aliyejiua kwa heshima, wafunguka haya


KANISA Katoliki limesema mtawa Suzan Bartholomew (48), aliyefariki dunia baada ya kujirusha chini kutoka ghorofa ya pili ya moja ya majengo ya Hospitali ya Bugando, amezikwa kwa heshima zote za kanisa kwa sababu alipata nafasi ya kutubu kabla umauti haujamfika.

Mara baada ya taarifa za kujiua kwa mtawa huyo kutolewa, mkanganyiko ulitokea ikiwa ni je atazikwa kwenye makaburi ya watawa ama laa kwani katika imani ya dini yake, mtu aliyejiua hukosa baadhi ya huduma wakati wa maziko yake.

Suzan ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando (BMC), anadaiwa kujirusha ghorofani usiku wa kuamkia Agosti 27,2018.

Alilazwa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) na kuendelea kupatiwa matibabu, lakini alifariki dunia usiku wa Agosti 28, wakati akiendelea kutibiwa.

Inadaiwa alichukua uamuzi wa kujirusha ili kujiua kutokana na sakata la upotevu wa Sh milioni 380 ndani ya kipindi cha miezi miwili katika idara ya uhasibu ndani ya kitengo chake.

Kutokana na sakata hilo, maofisa kadhaa walisimamishwa kazi, huku yeye akikamatwa na Jeshi la Polisi kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana.

Jana, Padri Deodadus Kagashe alisema Suzan alizikwa jana asubuhi katika makaburi hayo ili kutoa nafasi ya kuendelea na maandalizi ya mapokezi ya mwili wa Askofu Nestor Timanywa aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki.

Akielezea sababu za kupata huduma za misa, mmoja wa watawa wa Shirika la Theresia ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini, alisema Suzan alipatiwa huduma zote za misa wakati wa maziko yake kutokana na kupata wasaa wa kutubu kabla ya kufariki dunia.

“Ni kweli hakuna misa kwa watu wanaojiua bila ya kujali wadhifa wao, huyu alijirusha, hakufa papo hapo, alichukuliwa na kukimbizwa theater (chumba cha upasuaji), alitibiwa kutokana na kupata tatizo la spine code (uti wa mgongo), baada ya kupata nafuu na kujitambua aliomba huduma ya kanisa na kutubu,” alisema mtawa huyo.

Alisema japokuwa hawawezi kujua alitubu nini, lakini baada ya kitendo cha kujaribu kujiua kwa kujirusha kukwama, alichukuliwa akiwa hai, hivyo wakati akipatiwa matibabu aliomba kutubu na kupatiwa mpako wa wagonjwa, hivyo alifariki kikristu.

Alisema amezikwa kikristo na kupata huduma zote, kutokana na kutubu na kubainisha kuwa vinginevyo angezikwa kawaida kutokana na misimamo na misingi ya kanisa kwa watu wanaojiua kutopatiwa huduma ya misa.

“Juzi alfajiri tulimuaga Suzan kwa ibada ya misa na jana tumemzika, unajua watu wengi walitaka kujua atazikwaje kutokana na msimamo wa kanisa kutowafanyia ibada waumini au watawa wanaofariki kwa kujiua, lakini kifo cha huyu ni tofauti kwani alipata nafasi ya kutubu kabla ya kifo, hivyo amezikwa kwa heshima zote sawa na Wakristo wengine,” alisema.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC), Lucy Mogela, alisema mtawa huyo aliagwa kabla ya kusafirishwa kwenda Bukoba kwa misa iliyofanyika katika Kanisa la Bugando, lakini hakutaka kufafanua zaidi kwa madai kuwa utaratibu wote na masuala mengine yatatolewa na mkuu wa shirika lake.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari ya Jimbo Kuu la Mwanza, Padri Titus Ngapemba, alisema suala kuhusu taratibu na ibada ya mtawa Suzan linapaswa kutolewa ufafanuzi na Mkuu wa Shirika la Theresia aliyeko Bukoba.

Alipoulizwa iwapo Suzan alistahili kupata misa ya kumuaga na ile ya maziko, alisema ni kweli katika utaratibu wa Kanisa Katoliki huduma ya misa kwa mtu aliyejiua haitolewi na kueleza kuwa utaratibu wa mtawa huyo ulikuwa tofauti kwani maelezo aliyopata alitubu kabla ya kifo.

“Naomba nisiingie ndani, hayo unayoniuliza nadhani ukiwasiliana na Mkuu wa Shirika la Theresia utapata ufafanuzi, ninaweza kukueleza kwa ufupi kuwa mtu yeyote akifariki moja kwa moja kwa kujiua ni kweli hapati huduma, sasa hii ni tofauti na Sister Suzan, alijirusha hakufa papo hapo, hivyo naambiwa alipata wasaa wa kutubu, hivyo alizikwa kwa heshima zote za kikristo, mengine mtafuteni msimamizi wa shirika lake utaelezwa zaidi,” alisema.

Hata hivyo, Mkuu wa Shirika la mtawa huyo la Mt. Therisia, Hyasinta Misingo, hakupatikana kutokana na kudaiwa yupo kwenye majukumu mengine ya mapokezi ya mwili wa Askofu Timanywa.

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo kwani alikuwa kwenye msafara wa mazishi ya Askofu Timanywa na kuahidi kulitolea ufafanuzi zaidi leo iwapo bado utahitajika.

“Sasa hivi nipo kwenye msafara wa mapokezi ya mwili wa Askofu Timanywa, niulize ya askofu, hayo ya Suzan kesho nitapata wasaa wa kuyazungumzia,” alisema Askofu Kilaini.