Uongozi wa Simba kupitia kwa Ofisa Habari wake, Haji Manara, umeibuka na kukanusha taarifa za kuachana na Kocha wake Msaidizi, Masoud Djuma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti la Championi jana Jumatatu, ilieleza kuwa Djuma amekuwa hana maelewano na Kocha Mkuu, Patrick Aussems jambo ambalo linaweza kumng'oa klabuni hapo.
Aidha, Championi lilieleza kuwa Djuma anaweza akaondoshwa kutokana na kutengeneza migogoro baina ya wachezaji wa Simba na Kocha Aussems ili yeye aweze kuwa Kocha Mkuu.
Baada ya chapisho hilo kutoka, Manara ameibuka na kueleza kuwa hazina ukweli wowote na badala yake akasema bado Djuma ataendelea na majukumu yake kama Msaidizi wa Aussems.
"Taarifa hizo hazina ukweli wowote, bado Djuma ataendelea na majukumu yake, hakuna ambaye atakaa na Simba milele, kila mtu ataondoka kwa taratibu maalum pale muda utakapofika" alisema.
Mbali na Championi kuchapisha, taarifa hiyo iliandikwa kupitia mitandao mbalimbali ikiwemo blog hii.