F Ajali ya MV Nyerere yawaibua Polisi, yatoa tahadhari | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Ajali ya MV Nyerere yawaibua Polisi, yatoa tahadhari


NA TIMOTHY ITEMBE, TARIME
ZIKIWA zimepita siku chache baada ya kivuko cha MV Nyerere kuzama na watu zaidi ya 225 kupoteza maisha Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani mkoa wa kipolisi Tarime na Rorya wameomba wasafiri kutoa ushirikiano kwa vyombo husika pale ambapo kunatokea hitilafu ama uvunjifu wa sheria za usalama barabarani.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mrakibu wa Jeshi la Polisi Tarime na Rorya, SP, Ally Shaal alisema kuwa baadhi ya wasafiri wa kutumia vyombo vya usafiri wa nchi kavu na majini hawatoi ushirikiano kwa vyombo husika pindi wanapoona kero na uvunjifu wa sheria kwa watoa huduma wa vyombo hivyo kuwa na hitilafu.

" Ndugu waandishi wa habari kwanza nitoe pole kwa waathirika na majeruhi pamoja na kwa ndugu waliopotelewa na wapendwa wao kwenye  Ajali ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 20,2018 na watu zaidi ya 225 wakapoteza maisha niseme kuwa wasafiri wanatakiwa kutoa taarifa pindi wanapokuwa wameona makosa yanatendeka ndani ya vyombo wanavyotumia katika kusafiria ili wahusika wachukue hatua kabla ya matukio ya ajali kutokea" alisema Shaal.

Shaal aliongeza kuwa katika mkoa wake amebaini kuwa baadhi ya wasafiri wanayo tabia ya kuwalinda wamiliki wa vyombo pamoja na waajiriwa ambao wanahudumu wakati wa safari na hata wanapoulizwa na askari kama wako salama wao hujibu ndiyo hata kama kuna tatizo.