F Karia amwangukia Dk. Mengi, wadau | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Karia amwangukia Dk. Mengi, wadau

RAIS WA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA (TFF), WALLACE KARIA.

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amewataka wadau mbalimbali nchini kujitokeza kushirikiana na Mlezi wa timu ya Taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), Dk. Reginald Mengi kuisadia timu hiyo iweze kufikia malengo yake.

Karia alisema hayo jana wakati alipotembelea katika ofisi za Dk. Mengi akiwa na Kaimu Rais wa TFF, Athumani Nyamlani na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidao.

Serengeti Boys itakuwa mwenyeji wa mashindano ya vijana ya Afrika (AFCON-17) ambayo yanatarajiwa kuchezwa hapa jijini Dar es Salaam Aprili mwakani.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Karia, alisema kuwa Dk. Mengi anahitaji kuongezewa nguvu katika kufanikisha malengo ya Serengeti Boys yanatimia.

"Tunawaomba wapenzi na wadau wa soka kumsaidia Mzee Mengi kuilea hii timu, tunahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali kwa ajili ya kufikia malengo mazuri tuliyonayo," alisema Karia.

Rais huyo alivitaka vyombo vya habari kuendelea kuitangaza vyema Serengeti Boys na kwa kufanya hivyo itawavutia zaidi wadau na mashabiki kuipenda.

"Vyombo vya habari ni muhimu, tunawahitaji muendelee kuiandika vizuri Serengeti Boys, tunawaomba wadau wengine wasisite kujitokeza timu hii ambayo inapeperusha bendera ya nchi," alisema Karia.

Dk. Mengi alisema kuwa anaamini hakuna kisichowezekana na huu ni mwaka wa Watanzania kuonyesha uwezo wetu.

"Huu ni mwaka wa Watanzania, tunaweza kwenda Kombe la Dunia, huu ni wakati wa Tanzania...tutafanya kila tuwezalo, tutawapa malezi mazuri wachezaji wetu, nina imani na vijana hawa, tunaweza," alisema Dk. Mengi.