Na John Walter-Babati
Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018 Charles Francis Kabeho amezindua kiwanda cha Pombe kali cha Mati Super Brand L.t.d mradi ambao umegharimu shilingi Milioni 120.
Aidha Halmashauri ya mji wa Babati inaendelea Kusimamia uanzishaji viwanda ambapo mpaka sasa imefanikiwa kuwa na viwanda 13 kikiwemo cha Pombe kali Mati Supe Brand L.t.d ambacho kipo kata ya Bagara mtaa wa Bagara ziwani eneo la Korongo mbili kinachomilikiwa na watanzania watatu.
Mkurugenzi mtendaji David Damian Mlokozi amesema mwenge umewapa heshima kubwa kwa kuzindua kiwanda chao kwani ni ishara kuwa mheshimiwa rais amezindua.
“Sisi Kama Mati Super Brand L.t.d tumeitikia wito wa Rais John Pombe Magufuli kuwa na Tanzania ya Viwanda, sisi tumeanzisha kiwanda na kiwanda kitakwenda kuanzisha viwanda”alisema David.
Mr David amesema kiwanda chao kipo karibu na serikali kwa sababu hawana ujanja ujanja wanafuata taratibu zote za ulipaji kodi zinavyoelekezwa .
Taarifa ya kiwanda hicho kwa kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa ilieleza kuwa kiwanda hicho kimeweza kutoa ajira za kwa vijana 50, 19 za muda mfupi na 31 za kudumu.
Kuhusu kodi taarifa hiyo imefafanua kuwa, Kiasi cha shilingi milioni 154 kimelipwa serikalini tangu March hadi July mwaka huu.
Mbio za Mwenge ambazo kauli mbiu kwa mwaka huu ni ‘Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa zitahitimishwa Oktoba 14,2018 mkoani Tanga.