Katika biashara za zama hizi, usikae tu katika biashara yako ukingojea wateja waje kutoka kusikojulikana. Unatakiwa ufanye kazi ya kuwaleta wateja kwa mujibu wa uwezo wako na aina ya biashara unayo miliki ili kuzidisha mauzo na faida.
Machache katika haya yanafaa kuyafuata ili yasaidie kama mwongozo wa njia ya kuwavutia wateja zaidi na kufikia ongezeko la mauzo.
Namna ya kulielewa Soko
Kitu kikubwa cha msingi kujua ni kuelewa soko la bidhaa na huduma unayouza kwa uhakika. Ujue unakusudia kumuuzia nani na ana tabia gani ili ujue unamuuziaje. Soko ni watu utakao wauzia bidhaa na huduma. Ni wale ambao utawatengezea mikakati ya kuwafanya wanunue bidhaa na huduma zako.
Hii itasaidia vitu vingi ikiwamo wepesi wa kupanga mashambulizi ya kutangaza bidhaa na huduma ambayo yatafanana na aina ya soko ulilonalo.
Wafanyakazi Bora
Wafanyakazi ni sehemu kubwa ya kuwavutia wateja kuja kufanya manunuzi katika biashara yako. Tafuta wafanyakazi bora na siyo bora wafanyakazi.
Pia unaweza kuwatengeneza wafanyakazi waliopo wakawa bora zaidi kwa kuwapa programu mbalimbali za biashara.
Wafanyakazi ni uso wa biashara yako,bidhaa zako na jina la biashara yako. Wateja wanatarajia kufanya manunuzi kwa raha na huduma bora hivyo ni juu yako kuwafanya wafanyakazi wafanye kazi kwa umahiri ili kuwaridhisha wateja.
Inasaidia pia kuwafanya wafanyakazi wako watambulike na kujulikana kwa kuvaa sare ama kupatiwa vitambulisho au kuvaa lebo za majina yao na vyeo.
Ukaribisho pia unalipa kwa kuwafanya wateja wajisikie kuthaminiwa na kutambuliwa uwapo wao. Jitahidi wateja wako wajisikie vizuri kwa kupata ukaribisho mzuri katika biashara yako. Wateja wanapoingia katika biashara ama ofisi yako wakaribishe vyema kwa maneno na tabasamu.
Mitandao ya Kijamii
Mitandao ya kijamii ina wateja wengi, ni sehemu isiyohitaji kuachwa bila kutumiwa kukupatia mapato. Tangaza biashara yako kupitia huko na upate wateja.
Mitandao hii ipo mingi na inafikika kwa urahisi na watu wengi saa 24 kwa siku saba. Matumizi yake ni rahisi na gharama ni nafuu.
Acha kutumia mitandao hiyo kwa kupotezea muda wako, ongeza wateja kupitia mitandao ya kijamii.
Kuna namna nyingi ya kutumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara na huduma, miongoni ni; kutangaza ofa mbalimbali za biashara zako, kusambaza ujumbe wa punguzo la bei na kusambaza picha za bidhaa na bei zake.
Pia waweza kusambaza video zenye ujumbe unaoshawishi wateja waje kununua bidhaa zako na uwajulishe uwapo wa bidhaa mpya na kujibu maswali yao mbalimbali kuhusu bidhaa na huduma uzitoazo na hata ikiwezekana, tumia mitandao hiyo kutangaza nafasi za kazi kama unauhitaji wa kuajiri watu wa kukusaidia kufanya kazi kwenye duka lako au eneo lako lolote la biashara, kwa kufanya hivyo, watu wengi watatembelea akaunti zako na huko watapata fursa ya kuona bidhaa uziuzajo na kujua beia zake.