F Ugonjwa wa Pumu ni nini, Ufahamu Chanzo, Dalili na Tiba yake | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Ugonjwa wa Pumu ni nini, Ufahamu Chanzo, Dalili na Tiba yake


Utangulizi 
Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa ambao huathiri sehemu ya kupitisha hewa kwenda kwenye mapafu ya binadamu zinazojulikana kitaalamu kama bronchioles. Mtu mwenye pumu huwa na mcharuko mwili sugu (chronic Inflammation) kwenye mirija yake ya

kupitishia hewa (bronchioles tubes) hali ambayo husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hii, kujaa kwa ute mzito (mucus) na kupungua kwa njia ya kupitishia hewa, hali ambayo humfanya muathirika kushindwa kuvuta na kutoa hewa

nje na hivyo kupumua kwa shida sana. Hali hii inaweza kudumu kwa muda mfupi au mrefu kiasi cha kuhitaji tiba ili kumuwezesha mgonjwa kupata nafuu. Kutokana na kuwepo kwa msuguano na uzuiaji wa kupitisha hewa wakati wa kupumua hwa nje, pumu hujulikana pia kama obstructive lung disease . Mtu aliye na pumu, huwa nayo kipindi chote cha maisha yake.

Makundi ya Pumu

Pumu inaweza kugawanywa katika makundi mawili;
Pumu ya ghafla (Acute asthma): Wagonjwa wanaopatwa na kundi hili la pumu huwa na hali ya kawaida katika njia zao za hewa isiyobadilika kati ya shambulizi moja na jingine.

Pumu sugu (Chronic Asthma): Kundi hili la pumu huwa na tabia ya kuwa na njia nyembamba za kupitisha hewa na kadiri jinsi mgonjwa anavyoendelea kupata matukio zaidi ya pumu, njia za hewa huzidi kuwa nyembamba zaidi.

Aina za ugonjwa wa pumu 
Bila kujalisha mgonjwa anaingia katika kundi gani, ugonjwa wa pumu unaweza kugawanywa katika aina kuu nne, ambazo ni 1.Pumu inayobadilika (brittle asthma): Kulingana na tabia ya kujirudia rudia kwa matukio ta ugonjwa huu na madhara yake kwa mgonjwa, aina hii ya pumu inaweza kugawanywa zaidi katika aina nyingine mbili,

ambazo ni 
Aina ya kwanza ya pumu inayobadilika (type 1 brittle asthma) ni pumu yenye tabia ya kuwa na matukio na mashambulizi ya kubadilika kila mara japokuwa mgonjwa anaweza kuwa anapata matibabu kadhaa.

Aina ya pili ya pumu inayobadilika (type 2 brittle asthma) ni pumu ambayo mgonjwa anatokea kupata shambulizi la ghafla (asthmatic attack) wakati hapo awali ugonjwa wake uliweza kuthibitiwa kwa matibabu.

2. Pumu hatari isiyobadilika (status asthmaticus): Hii ni aina ya pumu iliyo hatari zaidi kwa mgonjwa. Pamoja na matumizi ya dawa kadhaa,zikiwemo vitanua njia za hewa (bronchodilators) na vipoza mcharuko mwili (steroids), mgonjwa wa aina hii ya pumu anaweza asipate nafuu ya haraka, na anaweza kupoteza maisha.

3.Pumu inayosababishwa na mazoezi (Exercise Induced Asthma): Hali hii husababishwa na ufanyaji wa kupitiliza wa mazoezi ya viungo. Kwa kawaida wakati wa kufanya mazoezi mtu hupumua kwa kutumia pua na kupitia mdomoni.

Hata hivyo wakati mwingine hutokea hewa aivutayo huingia ndani ikiwa haijapozwa vya kutosha puani na hivyo kusababisha ongezeko la mtiririko wa damu katika mishipa inayosambaza damu katika mirija ya kupitisha hewa. Hali hii husababisha kuvimba

kwa kuta za mirija hiyo na muhusika kupata shambulizi la pumu. Aina hii ya pumu yaweza kudhibitiwa na dawa. Inashauriwa sana kwa watu wenye matatizo kama haya kupasha moto misuli kwa mazoezi mepesi (warming up) kabla ya kuanza mazoezi mazito na ya muda mrefu. 4.Pumu inayosababishwa na aina ya kazi afanyayo muhusika (Occupational Induced Asthma): Wakati fulani, mazingira ya kazi yanaweza kusababisha kutokea kwa pumu hata kwa baadhi ya wafanyakazi wasio na tatizo hili. Mara nyingi aina hii huweza kuwatokea watu wanaofanya kazi kwenye viwanda vya kutengeneza matairi, vigae, rangi, kemikali mbalimbali, mbolea, chuma, unga na mbao.

Pumu husababishwa na nini? 
Kuna mambo kadhaa yanayoweza kusababisha kutokea kwa pumu au yanayohusishwa na shambulizi lake.

Mambo hayo ni pamoja na 

Matatizo ya kinasaba: Matatizo ya kinasaba yamehusishwa na kutokea kwa karibu asilimia 90 ya ugonjwa wa pumu hususani kipindi cha utoto.

Uvutaji wa sigara au tumbaku kipindi cha ujauzito pia unahusishwa na kusababisha pumu kwa mtoto atakayezaliwa.

Maendeleo ya kiuchumi: Ugonjwa wa pumu umeonekana sana kwenye nchi zilizoendelea kiuchumi ikilinganishwa na nchi zenye maendeleo na hali duni ya kiuchumi.

Magonjwa ya mapafu kama bronchitis
Vyanzo vya mzio (allergens)kama vile vumbi, vinyesi vya wanyama na baadhi ya vyakula.
Uchafuzi wa mazingira kama moshi na baadhi ya harufu kali.

Baadhi ya kemikali kwenye maeneo ya kazi hasa kwenye viwanda kama vya rangi, chuma, sementi na vigae.

Baadhi ya wagonjwa wanaotumia dawa za kushusha shinikizo la damu zilizo katika jamii ya beta-blockers kama vile propanolol wapo katika hatari ya kupata shambulio la ugonjwa wa pumu.

Magonjwa kwenye mfumo wa kupumua yasabishwayo na baadhi ya virusi na bakteria kama vile rhinovirus, Chlamydia pneumonia au Bordetella pertusis.

Matumizi ya mapema sana ya baadhi ya dawa hasa antibiotiki kwa watoto yanaweza kubadilisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa na hivyo kumfanya mtoto kuwa katika hatari ya kupata pumu.

Ongezeko la msongo wa mawazo huweza kusababisha pumu na matatizo katika mfumo wa upumuaji
Upasuaji wakati wa kujifungua (caesarian section): Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa kujifungua kwa njia ya upasuaji huongeza uwezekano wa kupata pumu kwa vile njia hiyo yaweza kuathiri mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya maradhi.

Vihatarishi vya ugonjwa wa pumu 

  • Uwezekano wa kupata ugonjwa wa pumu huongezeka iwapo mtu 
  • Atakuwa na magonjwa ya mzio kama vile magonjwa ya ngozi (eczema) au homa isababishwayo na aina fulani ya vumbi (hay fever)
  • Atavuta chavu (pollen) kutoka kwenye maua au miti
  • Atajihusisha na uvutaji sigara
  • Ana historia ya ugonjwa wa pumu au mzio kwenye familia
  • Utumiaji wa dawa aina ya aspirin
  • Ana msongo wa mawazo
  • Ana uambukizi wa magonjwa ya virusi kamarhinovirus
  • Mazoezi
  • Anaishi sehemu zenye baridi
  • Ana matatizo katika njia yake ya chakula (Gastroesophageal reflux disease au GERD)



Dalili za ugonjwa wa pumu 

  • Dalili za ugonjwa wa pumu ni pamoja na 
  • Kuishiwa na pumzi na kupumua kwa shida (shortness of breath)
  • Kutoa sauti kama mtu anayepiga miluzi wakati wa kupumua (wheezing)
  • Kukohoa sana (chronic cough) hasa nyakati za usiku au asubuhi. Aidha kikohozi huambatana na kutoa makohozi mazito, yasiyo na rangi au yenye rangi ya njano.
  • Kubana kwa kifua.
  • Kwa mtu aliyepata shambulizi kubwa la pumu (severe asthmatic attack) anaweza kushindwa kuzungumza na pia kuwa na hali kama ya kuchanganyikiwa.


Vipimo na Uchunguzi

  • Pamoja na daktari kutaka kufahamu historia ya mgonjwa, anaweza pia kuamua kufanya vipimo vifuatavyo ambavyo vitamsaidia kufahamu chanzo na madhara ya ugonjwa wa pumu kwa muathirika. 
  • Kipimo cha damu (complete blood count) msisitizo ukiwa kwenye wingi wa seli za damu aina ya eosinophils ambazo uhusika na kuwepo kwa shambulio la mzio.
  • Kipimo cha kuchunguza uwezo wa mgonjwa kutoa hewa nje mara baada ya kuivuta (spirometery). Aina hii ya uchunguzi hufanyika kabla ya mgonjwa kupewa dawa kwa kutumia nebulizer.
  • Kipimo cha kuchunguza kiwango cha hewa ya oksijeni kilichopo kwenye damu ya mgonjwa (oximetry).
  • Kipimo cha kuchunguza uwezo wa mgonjwa kupumua hewa nje wakati wa shambulizi la pumu (Peak flow meter).
  • X-ray ya kifua kwa ajili ya kutofautisha pumu na magonjwa mengine yenye dalili za kufanana kama vile ugonjwa wa moyo (congestive heart failure), magonjwa sugu ya kuziba kwa njia za hewa (COPD kama vile chronic bronchitis na emphysema) na magonjwa mengine ya kuzaliwa kama vile cystic fibrosis.
  • Kipimo cha mzio cha ngozi (skin allergy test) kwa ajili ya kutambua aina ya mzio inayomsababishia mgonjwa shambulizi la pumu.


Matibabu ya Pumu 
Kwa ujumla matibabu ya pumu hujumuisha kuepuka visababishi vya ugonjwa huu na matumizi ya madawa kwa walio na hali mbaya. Aidha, kwa wanaopata ugonjwa huu kwa sababu ya msongo wa mawazo hupewa ushauri nasaha kwa ajili ya

kusaidia kutatua matatizo yanayowakabili. Vilevile inashauriwa kwa wenye tatizo hili, kuwa na dawa karibu muda wote kwa ajili ya matumizi pindi shambulizi litakapotokea. Pia inashauriwa sana kuepuka mazingira na hali za baridi ambazo

huweza kuchochea kutokea kwa shambulio la ugonjwa huu. Matibabu ya kutumia dawa hujumuisha matumizi ya dawa za kusaidia kupunguza na kuondoa makohozi (expectorants), dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa (bronchodilators), dawa za kuondoa mcharuko mwili kama vile cortisone ya drip (hasa wakati wa dharura) au nebulizer, na dawa za kuzuia

mzio (antihistamine drugs). Hata hivyo, kuna matibabu ya ziada kulingana na hali ya mgonjwa pamoja na kundi na aina ya pumu inayomuathiri mgonjwa. Kwa wagonjwa wenye pumu ya ghafla na wenye hali mbaya (acute asthma) matibabu hujumuisha matumizi ya dawa za kutanua mirija ya hewa (bronchodilators) pamoja na kuongezewa hewa ya

oksijeni, dawa za kutuliza mcharuko mwili (steroids) pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (intravenous muscle relaxants). Aidha kwa vile mara nyingi shambulizi hili laweza kuwa la hatari sana, mgonjwa hulazwa

hospitali na huongezewa hewa ya oksijeni, na kwa wagonjwa wasioweza kupumua kabisa, husaidiwa kufanya hivyo kwa kutumia mashine maalum iitwayo (mechanical ventilator). Kwa wagonjwa wenye pumu sugu, jambo la muhimu ni

kuepuka visababishi vya pumu na kuendelea na matumizi ya dawa zinazosaidia katika kutanua mirija ya hewa. Kwa wagonjwa wanaopata mashambulzi ya mara kwa mara wanaweza kushauriwa na daktari kutumia dawa kadhaa zikiwemo zile zinazopunguza mcharuko mwili (mast cell inhibitors, inhaled steroids au oral steroids), pamoja na dawa za

kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (muscle relaxants). Aidha ni vema pia kutibiwa na kuthibiti kutokea kwa magonjwa yote yahusuyo mfumo wa hewa. Matumizi ya chanjo ya magonjwa kama influenza na pneumococcal pneumonia nayo husaidia sana katika uthibiti wa kutokea kwa pumu. Ni vema pia kuepuka matumizi ya dawa za jamii ya beta-blockers kwa wagonjwa wenye shinikizo la damu na ambao pia wana pumu.

Nini madhara ya pumu kwa mama wajawazito? 
Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa takribani theluthi moja ya wajawazito wenye pumu hupata nafuu kipindi cha ujauzito, theluthi nyingine hupata matatizo kipindi hiki na theluthi iliyobakia huwa na hali ya kawaida kama kabla ya ujauzito.

Kwa kawaida dalili za pumu hujirudia kama awali miezi mitatu baada ya kujifungua. Dalili za pumu kwa mjamzito zinaweza kuwa mbaya zaidi kuanzia wiki ya 24-36 (mwezi wa sita mpaka wa nane). Ni mara chache sana mjamzito

anapata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua. Inakisiwa kuwa, ni asilimia 10 tu ya wajawazito wenye pumu wanaopata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua. Baadhi ya dawa zinazotumika wakati wa ujauzito na baada ya

kujifungua huongeza madhara ya pumu, hivyo ni vizuri kumueleza daktari kwamba una pumu kabla ya kupewa dawa. Aidha na si vyema kunywa dawa kwa mazoea. Wanawake wenye pumu isiyoweza kuthibitiwa kipindi cha ujauzito

hupata madhara ya kuzaa mtoto njiti (premature baby), kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo, kifafa cha mimba, shinikizo la damu (Hypertension), na iwapo atapata shambulizi hatari wakati wa ujauzito mtoto anaweza kufa kwa kukosa hewa ya oksijeni.


Ugonjwa wa Pumu ( Athma kwa watoto

Nini maana ya Pumu?
Pumu ni hali ambayo huathiri njia za hewa, njia hizi za hewa pia huitwa mirija ya kupumulia. Mirija hii huanzia kwenye njia ya hewa(trachea) hadi kwenye mapafu.

Mchakato wa kupumua kwa watoto walio wengi ni rahisi : Watoto huingiza hewa kupitia puani au mdomoni na hewa huingia kwenye njia ya hewa(trachea) na kuelekea kwenye mapafu. Lakini Kwa watoto wenye pumu, hupumua Kwa shida Kwa sababu njia ya hewa hushindwa kupitisha hewa kwa sababu ya njia yao kuwa imehathiriwa na hali ya pumu.

Shambulio la pumu (Asthma attack) ni nini?
Hii ni hali ambayo hutokea wakati njia ya hewa inapo vimba na kuwa nyembamba na inakuwa vigumu kwa hewa kuingia na kutoka kwenye mapafu. Wakati mwingine njia za hewa zinapokuwa zimevimba hutoa majimaji mfano wa makamasi, hali ambayo husababisha mchakato mzima wa mabadlishano ya hewa katika mapafu kuwa mgumu na hii hali ndo inapelekea tatizo zima la mtotoanapo patwa na pumu kushindwa kupumua vizuri.

Wakati ugonjwa huu unaanza, upumuaji kwa mtoto unaweza kuwa wa kawaida na kuonekana kama vile hakuna tatizo, Lakini kipindi ugonjwa unapoanza, unaweza kuhisi kwamba mtu anapumua kupitia kwenye mrija. Mtoto mwenye pumu anaweza kutoa mlio kama wa filimbi (anapopumua), kukohoa, na kusikia kifua kubana.

Wakati shambulio la ugonjwa wa pumu(asthma attack), hali inaweza kuwa mbaya zaidi kama mtoto hatatumia dawa sahii za pumu. Baada ya kutumia dawa na kupata matibau sahii wakati wa shambulio la ugonjwa wa pumu, njia ya hewa mara nyingi hurudia hali yake ya kawaida, ingawa inaweza kuchukua muda mrefu kidogo wakati mwingine.

Pumu huwapata watu gani?
Pumu ni ugonjwa ambao huwapata watu wengi zaidi ya unavyo weza kufikiri.Karibia watoto milioni sita nchini marekani wanaumwa ugonjwa wa pumu(Hatujui hapa kwetu Tanzania ni idadi gani?).Ugonjwa wa pumu humpata mtoto mmoja hadi wawili katika kila watoto 10 kwa marekani. Hii ina maana kwamba kama una watoto 20 darasani, watoto 2-4 kati yao wanaweza kuwa na ugonjwa wa pumu. Ugonjwa wa pumu unaweza kumshika mtu katika umri wowote- kuanzia mtoto mchanga hadi mtu mzima-lakini huwashika zaidi watoto wenye umri wa kwenda shule(kuanzia miaka sita na kuendelea)

Hakuna anayejua kwa uhakika kwa nini ugonjwa huu unampata mtu mmoja na kuacha mwingine, lakini tunajua kwamba ugonjwa wa pumu unatokea ndani ya familia zetu. Hii ina maana kwamba kama mtoto ana pumu, yeye pia anaweza kuwa na mzazi, ndugu, mjomba au jamaa mwingine mwenye pumu au alikuwa na ugonjwa huu wakati bado mtoto.

Ugonjwa wa pumu unapoanza,huonyesha kama vile ni mafua,ambayo huambatana na kikohozi chenye kutoa mlio wa filimbi,lakini ugonjwa wa pumu siyo wa kuambukizwa. Huwezi kuambukizwa Kama unavyopata mafua

Ni sababbu zipi zinazopelekea Kupata shambulio la ugonjwa wa pumu (Asthma attack)?
Visababishi hutofautiana kutoka mtoto mmoja hadi mwingine. Sababu zipo nyingi.Baadhi ya watoto huwa na mzio(allergy), kwa vile vitu ambavyo huathiri njia ya hewa. Mara nyingi vitu vinavyoleta mzio kwa watoto wenye pumu ni vijidudu vidogo jamii ya mchwa vinavyopatikana kwenye vumbi, harufu mbaya (kama ulikuwa karibu na dimbwi na kuvuta harufu hiyo), mbelewele(pollen) kutoka mitini, majani na kwenye magugu.

Watoto wengi hupata shambulio la pumu wanapokuwa karibu na wanyama wenye manyoya kama Paka na mbwa,baadhi watoto wanapovuta hewa iliyochanganyika na chembechembe za manyoya hawa wanaweza pata shambulio la pumu.

Visababishi vingine ni pamoja na marashi(perfumes), vumbi la chaki, na uvutaji wa sigara. Uvutaji wa sigara sio mzuri hasa kwa mtu mwenye pumu.

Wakati mwingine maambukizi mbalimbali yanaweza kusababisha kulipuka kwa ugonjwa wa pumu,maradhi kama mafua, Kwa baadhi ya watoto, hali ya hewa yenye baridi inaweza kusababisha kulipuka kwa ugonjwa huo,baadhi ya watoto hupatwa na matatizo ya pumu wanapokuwa wanafanya mazoezi,hii ni aina ya pumu inayosababishwa na mazoezi.

Jinsi gani unaweza kutibu ugonjwa wa pumu kwa watoto?
Watoto wenye ugonjwa wa pumu wanatakiwa kujaribu kuepuka visababishi vyote vinavyoweza kuwasababishia shambulio la hewa.Ingawa kuna baadhi ya visababishi kama vumbi la chaki ni vigumu kuviepuka katika mzaizngira yetu hasa shuleni,lakini mtoto,wazazi na walimu wajaribu kuwasaidia watoto wenye matatizo haya.

Sura ya ugonjwa wa pumu hutofautiana kutoka kwa mtoto mmoja hadi mwingine, hivyo kuna dawa mbalimbali za kutibu ugonjwa wa pumu,na matibabu haya hutofautiana kati ya mtoto mmoja na mwingine hii ni baada yake daktari kujaribu kufuatilia sababu zilizopelekea ugonjwa huo, ni kwa kasi gani ugonjwa umetokea, na kiwango cha madhara ya ugonjwa huo. Hapo ndipo ataamua tiba ipi itakuwa sahii na bora kwa mtoto.

Baadhi ya watoto wanatakiwa wameze dawa za pumu mara kwa mara punde wanapopata ugonjwa huu. Hii huitwa dawa ya dharura kwa sababu hufanya kazi ya kufungua njia ya hewa ili mtu aweze kupumua. Watoto wengine wanatakiwa kutumia dawa za kudhibiti ugonjwa wa pumu kila siku,Dawa hizi huzuia shambulio la ugonjwa(asthma attack) kutokea.Kwa hiyo matibabu ya Pumu yanatofautina kutoka mtoto mmoja na mwingine.

Kwa watoto walio wengi ugonjwa wa pumu hupona au hupata nafuu wanapokua wakubwa. Baadhi ya madaktari wanadai kwamba hii hutokea kwa sababu, njia ya hewa hupanuka kadri mtoto anavyokua mkubwa. Njia ya hewa inapopanuka, hewa huingia na kutoka kiurahisi

Baadhi ya watu wazima hupata ugonjwa wa pumu, lakini hii haiwasumbui.Wanariadha wengi katika mbio za olimpiki na magwiji wengine wa michezo wanaweza kuendelea na michezo hata wanapokuwa na ugonjwa wa pumu.

UJUMBE WA KUPELEKA NYUMBANI:
Mzazi au mlezi anayeona mtoto mwenye dalili za ugonjwa wa pumu kama nilivyouelezea hapo juu kitu cha kwanza cha kufanya ni kumwaisha Katika kituo chochote cha Afya au Hospitali iliyo karibu nae.

Na kwa wale watoto walikwisha gundulika tayari na ugonjwa huu wa Pumu ni kuhakikisha wanafuta masharti yote ya Matibabu ili kuzuia shambulio la ugonjwa huu.

Mtoto anayejua mapema kwamba kuna vitu vinamletea madhara katika njia ya hewa au sababu nyingine anaweza kutumia dawa mapema zitakazosaidia kufanya njia ya hewa iendelee kuwa wazi.Mtoto ambaye hupata pumu anapofanya mazoezi anaweza kutumia dawa kabla ya kufanya mazoezi ili waweze kumaliza mbio au michezo vizuri.

Kwa watoto walio wengi ugonjwa wa pumu hupona au hupata nafuu wanapokua wakubwa. Baadhi ya madaktari wanadai kwamba hii hutokea kwa sababu, njia ya hewa hupanuka kadri mtoto anavyokua mkubwa. Njia ya hewa inapopanuka, hewa huingia na kutoka kiurahisi

Baadhi ya watu wazima hupata ugonjwa wa pumu, lakini hii haiwasumbui.Wanariadha wengi katika mbio za olimpiki na magwiji wengine wa michezo wanaweza kuendelea na michezo hata wanapokuwa na ugonjwa wa pumu.