Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) limekifungia kiwanda cha kusindika nyama ya punda kilichopo jijini Dodoma baada ya ukaidi wa muda mrefu wa mmiliki kufuata taratibu sahihi za uhifadhi wa mazingira.
Barua iliyoandikwa na Kaimu Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Vedast Makota imeeleza kwamba kiwanda hicho ambacho kinashughulika na uchinjaji na usafirishaji wa nyama ya punda nje ya nchi kwa muda mrefu sasa kimeonyesha kushindwa kuzingatia taratibu za uhifadhi wa mazingiramlicha ya onyo na ukumbusho kadhaa uliofanywa na baraza.
“Kufuatia mlolongo huu wa uchafuzi wa mazingira ambao umekuwa ni kero kwa majirani na ambao unaleta shaka kwenye ubora wa bidhaa, Baraza limefikia hatua ambayo linakosa cha kushauri zaidi ya kufunga kiwanda,” ilieleza barua hiyo.
Kwenye maelezo ya ufungaji wa kiwanda hicho, Dk. Makota alisema:
“Kwa mamlaka yaliyokabidhiwa kwa Baraza chini ya Kifungu cha 196(2) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, unaamuriwa kusimamisha shughuli zote za uzalishaji kuanzia siku ya agizo hili mpaka utakapochukua hatua kikamilifu za kutekeleza maagizo yote uliyopewa hapo awali.”
Kiwanda hicho ambacho kinamilikiwa na kampuni ya Huwachen Company Limited kimekuwa kwenye mvutano wa muda mrefu na Baraza pamoja na Wizara inayohusika na uhifadhi wa mazingira tangu Mei, mwaka huu ambapo aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola, alitembelea na kueleza kutoridhishwa kwake na hali ya uhifadhi wa mazingira.
Ziara hiyo ya Lugola ilifuatiwa na ukaguzi wa NEMC uliofanywa Agosti mwaka huu kwa lengo la kutathmini hali ya uhifadhi wa
mazingira kwenye kiwanda hicho kutokana na shughuli zake. Katika tathmini hiyo suala la uchafuzi wa mazingira liliendelea kuonekana kuwapo.
Mambo yaliyoonekana kuwa ni tatizo ni pamoja na mabaki ya damu kwenye eneo hilo ambayo yalisababisha uwapo wa nzi wengi, kuziba kwa mitaro ya kupitisha maji machafu, kukosekana kwa utaratibu madhubuti wa kuhifadhi mbolea, kiwango duni cha shimo la kuhifadhia uchafu, harufu mbaya na ukosekanaji wa mpango endelevu.
Mapungufu hayo kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Mkurugenzi wa NEMC yanakiuka vifungu kadhaa vya sheria ya mazingira ya mwaka 2004, hii ni pamoja na kifungu cha 106 (1) (2) na (6) pamoja na kifungu cha 187 (1) (b) na (C).
Pamoja na maelekezo yaliyokuwa yametolewa na NEMC kwa kiwanda hicho, Baraza pia Agosti 10 lilikiamuru kiwanda hicho kulipa faini ya Sh. milioni 30 kama adhabu kwa kutokuzingatia uhifadhi mzuri wa mazingira, lakini adhabu hiyo haikutekelezwa.
Ukaguzi wa mwisho ulifanyika Oktoba 26 ambao ulifuatiwa na kufungwa kwa kiwanda hicho.