Na John Walter-Babati
Wanafunzi wanaohitimu fani mbalimbali katika vyuo vya ufundi stadi hapa nchini [VETA] wametakiwa kufuta dhana ya kuajiriwa na kukaa ofisini bali elimu walioipata waitumie kuweza kujiajiri wenyewe na kuiondolea serikali mzigo wa ukosefu wa ajira kwa vijana.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati Ndg. Fortunatus Fwema wakati akizungumza na wazazi,walimu na wanafunzi wanaohitimu mafunzo ya fani mbalimbali katika chuo cha VETA Manyara kwenye mahafali ya tano yaliyofanyika katika chuo hicho.
Fwema amewataka wahitimu kuweza kuyatumia vizuri maarifa waliyoyapata katika kubadilisha mazingira na kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika maisha yao binafsi,familia zao na taifa kwa ujumla kwani ndio dhamira ya serikali ya awamu ya tano.
Amesema “kwa bahati mbaya hapa Afrika na Tanzania in Particular, elimu tunayoipata ni ya Magharibi mno,elimu ambayo inatutaka twende maofisini,tuajiriwe na hivyo inatutoa nje ya mzunguko halisi ya matatizo yetu yanayotukabili,chuo cha VETA ndio muarobaini wa mtazamo huo kwa sababu chuo kinatoa wataalamu ambao wanaenda kujiajiri”.
Nao wahitimu wa fani mbalimbali wamesema baada ya mafunzo hayo chuoni hapo watahakikisha wanawatendea haki wote wanaowategemea pamoja na nchi inayosisitiza wanafunzi kujiajiri baada ya kutoka vyuoni badala ya kuwa tegemezi kwenye famiulia zao na kuisubiri serikali iwape ajira.
Kwa upande wake mkuu wa chuo cha hicho cha Ufundi Stadi VETA Manyara Mwalimu Felix Orundukai, amesema chuo kinakabiliwa na uhaba wa madarasa kwa ajili ya masomo bebezi na mtambuka na pia idadi ya maombi ya kujiunga na chuo ni makubwa ukilinganisha na uwezo wa chuo.
Pia amesema chuo kimefanikiwa kupata shilingi milioni 200,000,000 kutoka makao makuu VETA kwa ajili ya ujenzi wa Karakana ya Uashi huku ikisisitiza kufuata taratibu zote za manunuzi katika kukamilisha ujenzi huo ambao ulisimamiwa na Wakala wa majengo [TBA].
Amesema mradi wa ujenzi wa karakana hiyo ya VETA Manyara unakadiriwa kutumia kiasi cha Fedha Milioni 300,000,000 badala ya shilingi milioni 500,000,000 kama jengo hilo lingejengwa na mkandarasi
Aidha amesema kiasi cha shilingi milioni 200,000,000 imepelekwa kwa ajili ya kazi ya ujenzi ambapo mpaka sasa kiasi kilichotumika ni shilingi 190,000,000 huku akieleza kuwa wamefanikiwa kwenda sambamba na malengo waliojiwekea na kusimamia manunuzi na kazi kwa kuhakikisha inafanyika kwa gharama nafuu na kwa ubora wa hali ya juu.
Wanafunzi 175 wa fani mbalimbali wanatarajia kufanya mitihani yao mwanzoni mwa mwezi Desemba 2018 kati ya wanafunzi 205 huku wengine 30 wakishindwa kuendelea kwa sababu mbalimbali.
Chuo cha VETA Manyara kilianza na jumla ya wanafunzi 98 ambapo wasichana walikuwa 18,wavulana 80 mwaka 2012 na katika mwaka 2018 chuo kina jumla ya wanafunzi 405 wa fani za muda mrefu ambapo kati yao wasichana ni 107 na wavulana ni 298.