Uongozi wa Yanga umesema kuwa kwa sasa upo kwenye hatua nzuri ya mazungumzo na baadhi ya timu kutoka Ulaya ambazo zinawafuatilia kwa ukaribu wachezaji wao ili waweze kwenda kujiunga na timu zao kuongeza uzoefu zaidi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hussen Nyika amesema kuwa mipango inakwenda vizuri kwa kuwa wana mawasiliano ya karibu na timu za nje ya nchi ambazo zinawataka wachezaji wao.
"Kuna wachezaji watatu ndani ya Yanga ambao wanatakiwa kwenda kucheza nje ya nchi, kwa kuwa mazungumzo ya awali yamefanyika, kinachosubiriwa kwa sasa ni barua tu ili jambo hili liweze kukamilika na kutangazwa.
"Tunapenda kuona wachezaji wakipata mafanikio hasa kwa kuweza kucheza nje ya nchi jambo ambalo linaongeza thamani ya mchezaji pamoja na kuongeza wachezaji wa kimataifa ambao ni hazina kubwa ndani ya taifa letu hivyo wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi," alisema.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema kuwa wachezaji wake wengi wana uwezo wa kucheza nje ya nchi kwa kuwa wanajituma na wanajua kazi ya kufanya hasa wakipewa maelekezo.
"Tuna wachezaji wengi wenye vipaji na wanaweza kucheza ulaya, Ibrahim Ajibu, Feisal Salum 'Fei Toto' na huyu Paul Godfrey ambaye ni chipukizi anakuja vizuri ana kitu ambacho anacho, hawa wote wakiongeza juhudi wanaweza kupata timu nje ya nchi na wakafanikiwa kufanya vizuri," alisema.