Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philipo Mpango amesema kuwa misaada kutoka katika nchi ambazo Tanzania ilikuwa inategemea imeteremka na iliyobaki ina masharti makubwa na ya hovyo.
Dkt. Mpango ameyasema hayo leo wakati akifunga mkutano wa mwaka wa kwanza wa watumiaji wa mfumo huo uliofanyika katika ukumbi wa Kambarage Jijini Dodoma
Kufuatia hali hiyo Dkt. Mpango amewataka watumiaji wa mfumo wa GePG katika ukusanyaji wa fedha za Umma kuwa wazalendo katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na usimamizi dhabiti wa mfumo huo wa GePG ili nchi iweze kujisimamia katika mapato ya ndani.
Dkt.Mpango amesema kuwa anatamani ifike siku moja aseme kuwa sasa serikali yetu inajitegemea na kujiendesha kwa asilimia 100, tofauti na hivi sasa ambapo bado tunautegemezi japo kwa kiwango kidogo, ifike hatua tuchukue mikopo na si fedha za msaada.
Waziri amesema kuwa lazima kujitegemea kama nchi na ili kufanikisha hilo, ni lazima serikali kuu na serikali za mitaa wajielekeze kusimamia mapato.
“Yani bila haya wala aibu wanaotaka kutupa misaada wanafikia hatua ya kusema eti tukubali ushoga ndipo watusaidie, ninyi mnaona hiyo ni sawa, mko tayari kwa hili, haiwezekani kamwe kuuza utu wetu,”amesema Dkt.Mpango
Aidha Dkt. Mpango amesema kuwa kumekuwa na kauli za ajabu za kubeza na kukatisha tamaa kazi kubwa ya kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato inayofanywa katika nchi, inayofanywa na serikali ya awamu ya Tano.
Amesema Serikali inapoamua kudhibiti madini wanasema wanafukuza wawekezaji, “Je mpo tayari tuache waendelee kufanya ufujaji huo, kwa miaka 50 waliyofanya mambo hayo kwa sasa inatosha, tuseme basi na tusonge mbele,”amesisitiza Dkt.Mpango
Hata hivyo Dkt.Mpango amefafanua kuwa nchi inapoamua kupeleka majeshi kuthibiti magendo, wanasema wanarudisha nyuma biashara ya usafirishaji hapa nchini.