Na John Walter-Manyara
Imeelezwa kuwa mitindo ya maisha wanayoishi wengi na kutofanya usafi wa meno na kinywa mara kwa mara ni kisababishi kikubwa cha Matatizo ya Meno na Kinywa.
Hayo ameyasema Daktari bingwa wa magonjwa ya Kinywa na meno Dr. Venant Vedasto wakati alipokuwa akitoa huduma ya kibingwa kwa wakazi wa Manyara iliyofanyika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara wiki iliyopita ambapo walibaini kuwa wengi waliokuja kupatiwa matibabu hayo waligundulika kuwa meno yao yametoboka kutokana na kula vyakula vyenye sukari kwa wingi na wengine wakiugua magonjwa ya fizi.
Amesema ukanda wa Arusha,Kilimanjaro na Manyara watu wengi meno yao yana Floride nyingi hali ambayo bila kuzingatia kanuni za usafi wa meno na Kinywa hupelekea kutobolewa kwa meno kirahisi na hali hiyo huanzia matumizi ya maji hayo tangu utotoni.
Amesema matumizi ya sukari kwa wingi mbali na kusababisha meno kuoza lakini pia ndio chanzo cha magonjwa ya Presha na Kisukari hivyo ni wakati wa watu wanaoendekeza maisha ya starehe kula vitu vyenye sukari kwa wingi kuacha ili kuepuka hali hiyo.
Madaktari bingwa nane wa magonjwa mbalimbali walifika mkoani Manyara na kutoa huduma mbalimbali ambapo wananchi zaidi ya 600 walisikilizwa na kutibiwa huku hitaji la madaktari hao likionekana kuhitajika zaidi na wananchi kwani wengi wamekuwa wakisumbuliwa na maradhi lakini wanakosa hata nauli ya kusafiri kufuata huduma.
Upande wa watoto waliofika kutibiwa, Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto Dr.Judith Cosmas ameeleza kuwa wengi wao wanalalamika kuumwa tumbo,njia ya mkojo,njia ya upumuaji.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani Dr. Smitha Balya kutoka hospitali ya Jakaya Kikwete anasema zaidi ya asilimia 70% ya wagonjwa aliowahudumia wanasumbuliwa na Magonjwa ya moyo kutanuka kutokana na tatizo kuwa la muda mrefu.
Dr.Balya amesema bado kazi kubwa inahitajika kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Magonjwa ya Presha na kisukari kwa kuwa wengi wanaotumia dawa wanazopatiwa huacha pindi wanapoona nafuu hali inayosababisha ugonjwa kuanza upya.
Mfuko wa taifa wa bima ya afya [NHIF] uliamua kuanza kupeleka madaktari bingwa katika mikoa ya pembezoni baada ya kuona changamoto mbalimbali zinazoikabili ikiwemo miundo mbinu na wataalamu ambapo mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa hiyo.
Afisa mwandamizi wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Dr. Rafael Malaba amesema kabla ya kuleta madaktari hao wanakaa na mkoa husika ili kujua hitaji lao ambapo waliketi na uongozi wa mkoa kwa upande wa afya na viongozi wa serikali,Katibu tawala wa mkoa,Mkuu wa mkoa na kukubalina kuwa wanahitaji madaktari nane kwa ajili ya kutibu magonjwa yanayowakabili wananchi wa Manyara.
Huduma hizo za kimatibabu mkoa wa Manyara ilifunguliwa na mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu akiambatana na mwenyekiti wa Mfuko wa taifa wa Bima ya Afya Dr. Anna Makinda ambapo huduma ilitolewa kwa siku tano kuanzia tarehe 10 hadi 15 desemba 2018.