F Makala: Wasanii 10 wa Bongo Fleva waliofanya vizuri mwaka 2018 | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Makala: Wasanii 10 wa Bongo Fleva waliofanya vizuri mwaka 2018



Muziki wa Bongo Fleva ni kiwanda chenye wafanyakazi (wasanii) zaidi, wapo walioanza na kiwanda hiki mwanzo, wengine walijiunga katikati ya safari na  kuna wapya wanajiunga sasa. Wote hawa kazi yao ni moja tu, si nyingine  bali kutoa burudani kwa mashabiki wao ambao ndio wanunuzi wa bidhaa husika.

Kwa mwaka 2018 kila mmoja amefanya kazi kwa kiwango chake kutokana na malengo aliyojiwekea na wengine kadiri mazingira yalivyoruhusu. Vyovyote ilivyokuwa, napenda kuangazia wasanii 10 kutoka kwenye muziki hao ambao wamefanya vizuri zaidi kwa mwaka huu.

1. Harmonize

Mwaka 2018  umekuwa wenye mafanikio makubwa sana kwa Harmonize kimuziki ukilinganisha na miaka mingine. ametoa nyimbo ambazo zimefanya vizuri zaidi na pia ameweza kushirikiana na wasanii wakubwa kutoka Tanzania na mataifa mengine ya Afrika.

Muimbaji huyo ambaye ndiye msanii wa kwanza kusaini kwenye lebo ya Diamond Platnumz 'WCB' mwaka huu ameweza kufanya kolabo na wakongwe wa Bongo Fleva kama Dully Skyes na Professor Jay ambao wote wawili walishawahi kufanya kazi na Diamond 'Chibu Dangote' na kufanya vizuri.

Pia ameweza kufanya kazi na wasanii wakali kutoka Afrika kama Eddy Kenzo (Uganda), Marina (Rwanda), Willy Paul (Kenya), Sarkodie (Ghana). Wengine ni Emma Nyra, Skales, IYO na OmoAkin, wote kutokea Nigeria. 

Wimbo wake unaokwenda kwa jina la Kwangwaru aliomshirikisha Diamond unatajwa kama wimbo wenye mafanikio makubwa zaidi kwenye Bongo Fleva kwa mwaka huu, kivipi?.

Ndio wimbo pekee ulitazamwa zaidi kwenye mtandao wa YouTube kwa mwaka huu, hadi sasa una views  Milioni 38. Video ya wimbo huu ilitoka April 14, 2018 iliweza kuweka rekodi ya kufikisha views Milioni 10  kwa kipindi cha mwezi mmoja kitu ambacho hakuna msanii wa Tanzania aliyewahi kufanya hivyo.

Hapo awali wimbo wa Harmonize ulikuwa ukiongoza kutazamwa zaidi YouTube ni Bado ambao pia alimshirikisha Diamond. Wimbo huu ulitoka miaka miwili iliyopita na hadi sasa una views Milioni 20 na uliwekwa kwenye mtandao huo February 29, 2016.

Ukiachana na hilo pia Harmonie kwa mwaka amefanya ziara ya kimuiki (music tour) nchini Marekani kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja ambapo alifanya show zake Houston TX, Dallas TX, Oakland CA, Seattle WA, Atlanta GA, Los Angeles CA, Private Event na Washington DC.

2. Diamond Platnumz

Ni miaka mingi sasa amekuwa akifanya vizuri, kila mwaka amekuwa na nyimbo ambao zinafanya vizuri kwenye chati za muziki, tuzo, mtaani na mtandaoni (streaming), achana na hilo.

Kwa mwaka huu amesumbua na albamu yake mpya iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu 'A Boy From Tandale' ikiwa ni albamu yake ya pili tangu alipotoka kimuziki mwaka 2009.

Albamu ya  A Boy From Tandale ilizinduliwa rasmi March 14, 2018 Nairobi nchini Kenya ambapo wasanii wote kutoka WCB walishiriki pamoja na msanii kutokea Marekani, Omario ambaye pia ameshiriki kwenye wimbo wake unaokwenda kwa jina la African Beauty.

Wasanii kutoka nje ya Tanzania walioshiriki kwenye albamu hiyo yenye nyimbo 18 ni kundi la Morgan Heritage (Jamaica), Jah Prayzah (Zimbabwe), Omario, Rick Ross na Ne-Yo (wote Marekani), pia kuna Tiwa Savage, Davido, P Square na Mr. Flavour hawa wote kutokea Nigeria.
Licha ya albamu hiyo kutofanyiwa uzinduzi nchini Tanzania, Diamond alifanya ziara (tour) kwa ajili ya kuitangaza nchini Marekani kwa kipindi cha mwezi mmoja, wapenda muziki wa Afrika kutoka maeneo ya Texas, Los Angeles na Chicago walimpata mubashara kabisa Chibu  Dangote.

3. Vanessa Mdee

Umekuwa ni mwaka mwingine wenye mafanikio kwa muimbaji huyo wa kike wenye uwezo wa kuimba kwa ufasaha lugha zaidi ya tatu (Kiswahili, Kingereza, Kifaransa na Kihindi). Ni Vee Money au Cash Madam, licha ya kutoa nyimbo kadhaa ningependa kuangaza mafanikio yake katika mambo manne;

Mosi; Lebo, ukiachana na Diamond Platnumz na Alikiba, Vanessa Mdee pia ana lebo yake ya muziki inayofahamika kama Mdee Music ikiwa na wasanii watatu, Vanessa mwenyewe, Brian Simba na Mimi Mars.

Akiwa kama msimamizi mkuu wa lebo hiyo, Vanessa ameweza kumsimamia Mimi Mars na kutoa  EP yenye nyimbo sita na kuwa msanii pekee wa kike Tanzania kufanya hivyo kwa mwaka huu. Pia Mimi Mars anatarajiwa kuonekanekana kwenye msimu mpya wa Coke Studio Afrika.

Pili; mwaka huu Vanessa Mdee ametoa albamu yake ya kwanza, Money  Mondays tangu alipoanza muziki. Albamu hiyo yenye nyimbo 17 imefanya vizuri kimauzo kwa pande zote. Wasanii aliowashirikisha kwenye albamu hiyo ni kama Maua Sama, Joh Makini, Reekado Banks (Nigeria) Cassper Nyovest na AKA (Afrika Kusini).

Tatu;  Vanessa Mdee ni miongoni mwa wasanii watatu pekee wa Tanzania waliotumbuiza kwenye tamasha la One African Music kwa mwaka 2018.
Wasanii wengine kutoka Bongo walioshiri kwenye tamasha hilo lilofanyika November 16, 2018, Dubai, ni Nandy na Diamond.

Tanzania ndio nchi iliyotoa wasanii wengi Afrika Mashariki, Kenya iliwakilishwa na msanii mmoja, Akothee. Si mara ya kwanza kwa Vanessa kushiriki tamasha hilo ambalo limekuwa likikutanisha wasanii kubwa wa Afrika, hivyo muimbaji huyu anazidi kudumu na ukali wake.

Nne: ziara ya kimuki (music tour), kwa kushirikiana na Jux ambaye ni mpenzi  wake, mwaka huu wamefanya ziara yao iliyojulikana kama 'In Love & Money'. Ziara hii iliyopita kwenye mikoa ya Mtwara, Mwanza, Dodoma, Arusha na Dar es Salaan ilikuwa yenye mafanikio makubwa zaidi kwani kila walipoenda watu walifurika.

4. Maua Sama

Hakuna ubishi kuwa wimbo wa Maua Sama, Iokote umefanya vizuri zaidi kuliko nyimbo za wasanii wote wa kike zilizotoka ndani ya mwaka huu.
Ni wimbo wake wa tatu kutoa  ndani ya mwaka huu baada ya Nakuelewa na Amen ambao ameshirikiana na Ben Pol ukiwa pia ni wimbo wao pili kufanya pamoja. Iokote umekuja kuandika histori nyingine kwenye maisha ya kimuziki kwa upande wa Maua Sama, kivipi?.

Maua Sama amekuwa msanii wa kwanza wa kike Tanzania kwa wimbo wake kufikisha views Milioni 1 kwenye mtandao wa YouTube ndani ya wiki tatu bila video rasmi.  

Wakati anaweka rekodi hiyo alikuwa akishikiliwa na Jeshi la Polisi, Dar es Salaam kwa kile kilichoelezwa ni kusambaza video ya watu waliokuwa  wakicheza wimbo huo huku wakichezea fedha kwa kuzikanyaga kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo baada ya wiki moja alitoka na kutoa video rasmi ya wimbo huo ambayo pia imefanya vizuri kuliko video zake zote alizotoa tangu alipoanza muziki, hadi sasa ikiwa na views zaidi Milioni 5.7.

5. Mbosso

Huyo ni msanii wa mwisho kusainiwa na lebo ya WCB, usiku wa January 27, 2018 ndipo alitambulishwa rasmi na kutoa wimbo wake wa kwanza unaokwenda kwa jina la  Watakubali.

Utakumbuka baada ya kuvunjika kwa kundi la Yamoto Band kila msanii alianza kutoa kazi zake binafsi (solo project). Mbosso ndiye alikuwa msanii wa mwisho kutoa wimbo baada ya wenzake kumtangulia, hata hivyo amekuwa mwenye mafanikio makubwa zaidi.

Baada ya hapo ameweza kufanya vizuri na nyimbo kama Nadekezwa, Hodari, Nipepe na nyinginezo. Nyimbo hizi tatu nilizotaja, zote zina views zaidi ya Milioni 4.5 kwenye mtandao wa YouTube, si kitu kirahisi kwa muda huo tangu aliposaini WCB.

Pia imekuwa ni mapema kwake kufanya wimbo na Diamond Platnumz ukilinganisha na wasanii wengine wanaosaini kwenye lebo hiyo. Wimbo Jibebe waliofanya pamoja na Lava Lava ni miongoni mwa nyimbo chache kali zilizosumbua kila kona kwa mwaka huu.

6. Navy Kenzo

Ukiachilia mbali mahusiano ya kimapenzi waliyonayo na kama wazazi, hili ni kundi la waimbaji ambalo limefanya vizuri kwa mwaka huu. Wametoa nyimbo mbili pekee ambazo ni Fella na Katika na zote zimefanya vizuri.

Nyimbo hizi zimekuja mara baada ya kujaliwa kupata mtoto mmoja ambaye wamempa jina la Gold na kuchukua mapumziko mafupi kimuziki kwa ajili ya malezi, ujio wao mpya umekuwa wenye nguvu kubwa zaidi.

Wimbo wao uitwao Katika hadi sasa una views zaidi ya Milioni 8.8 kwenye mtandao wa YouTube tangu ulipotoka September 27, 2018. Pia wimbo huu  umeweza kushika nafasi ya kwanza kwenye chati za muziki za BBC Radio 1Xtra nchini Uingereza.

Utakumbuka producer Nahreel ambaye ni msanii wa kundi hili, mwaka huu pia ametengeneza wimbo wa Kombe la Dunia Russia 2018, wimbo huo ni ule  alioshiriki Diamond Platnumz na Jason Derulo kutoka Marekani. Huu ni wimbo wa tatu kwa Nahreel kufanya na Diamond baada ya Nana na Katika.

7. Alikiba

Licha ya kutoa nyimbo kadhaa na kufanya vizuri, kwa mara ya kwanza mwaka huu ameweza kutambulisha wasanii kutoka kwenye rekodi lebo yake 'Kings Music' ambayo ilikuwa ikizungumziwa kwa kipindi kirefu.
Kings Music kwa sasa ina wasanii wanne na Alikiba mwenyewe ambaye pia anafanya kazi na RockStar Africa akiwa kama Director of Music and Talents.

Utakumbuka July, 2017 Alikiba alitangazwa kuwa miongoni mwa wamiliki wa kampuni ya Rockstar4000 Music Entertainment Co & Rockstar Television ambayo kwa sasa inajulikana kama RockStar Africa.

King Music ndani ya mwaka huu wameweza kutoa nyimbo mbili ambazo ni Mwambie Sina na Toto. Alikiba si msanii wa kutoa nyimbo kila mara, kwa mwaka jana aliweza kutoa wimbo mmoja pekee, Seduce Me lakini kwa mwaka huu ametoa nyimbo mbili ambazo ni Mvumo wa Radi na Kadogo na zote  zimefanya vizuri.

Pia ameweza kufanya show kubwa ndani na nje ya Tanzania, moja wapo ni tamasha la Africa All Star Music Fest lilofanyika nchini Canada, August mwaka huu ambapo Alikiba alitumbuiza  jukwaa moja na wasanii kama Yemi Alade, Falz The Bahd Guy, Sheebah, Dj Spinal, Zahara, Nonso Amadi na Nsoki.

8. Nandy

Ukiachana na nyimbo kama Subalkheri Mpenzi na Aibu alizotoa kwa mwaka huu, pia huyu ni msanii wa pili wa kike Tanzania kutoa albamu kwa mwaka huu.

Ameweza kutoa albamu yake ya kwanza tangu kuanza muziki, The African Princess ikiwa na nyimbo 13 na ikiwa imemshirikisha msanii mmoja pekee ambaye ni Aslay. Albamu hii imeuzwa kwa mfumo wa nakala za kawaida (hard copy) pamoja na mtandaoni (streaming & downloads).

Pia ameweza kushinda tuzo mbalimbali kama African Entertainment Awards AEA USA 2018 zilizofanyika October 20, 2018, New Jersey nchini Marekani, Nandy alishinda kwenye kipengelee cha Best Single Female kupitia wimbo wake uitwao Kivuruge.

Huyu ndiye msanii pekee wa kike kutoka Tanzania kushinda tuzo hiyo kwa mwaka huu. Wasanii wengine walioshinda ni Diamond aliyechukua mbili kwenye vipengele vya vya Best Collaboration Of the Year kupitia wimbo wake, African Beauty, pia ameshinda kama Best Male Artist of the Year, huku Rayvanny akishinda kama  Best Vocalist of the Year.

Ukiachana na hilo mwaka huu kwa mara ya kwanza Nandy ameweza kushiriki tamasha la One African Music, Dubai. Amefanya show kadhaa nchini Marekani, pia anatarajiwa kuonekana kwenye msimu mpya wa Coke Studio Afrika.

9.  Rostam

Kundi hili la muziki wa hip hop linaloundwa na Roma na Stamina kwa mwaka jana liliweza kutoa nyimbo mbili ambazo ni Hivi Ama Vile na Kiba_100 ambao  ulikuja kufungiwa na Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) kutokana na kukiuka maadili, pia ulipelekea Roma kufungiwa kufanya muziki kwa kipindi cha miezi sita adhabu iliyokuja kuondolewa kabla ya muda huo.

Walianza mwaka kwa kuachia ngoma, Now You Know wakimshirikisha rapa kutoka nchini Kenya, Khaligraph Jones ambaye ameshafanya kazi na wasanii kadhaa wa Tanzania kama Rayvanny, Young Killer, Rosa Ree, Stereo na wengineo kibao.

Baada ya hapo wakatoa wimbo mwingine uitwao Parapanda ambao ndio umefanya vizuri zaidi kati ya nyimbo tatu walizotoa mwaka huu.  Licha ya kutotoa video ya wimbo huo, umeweza kufikisha views Milioni 1.5 katika mtandao wa YouTube tangu ulipotoka August 02, 2018.

Rostam ambao wanafahamika kwa kufanya show zenye ubunifu wa hali ya juu, mwaka huu wameendeleza hilo kwenye majukwaa mbalimbali makubwa waliyopanda kutoa burudani, pia ni kundi ambalo limefanya show nyingi zaidi kwa mwaka huu.

10. Weusi

Si mwaka huu pekee, kwa kipindi cha miaka kadhaa kundi la Weusi limekuwa likifanya vizuri na hata linapokuja sula la kutoa wimbo kwa msanii moja moja (solo project). Kundi hili ambalo linaundwa na wasanii watano, mara nyingi Joh Makini, Nikki wa Pili na G Nako ndio wamekuwa wakisikika zaidi lakini kwa mwaka huu wamebadili hilo.

Bonta na Lord Eyes kwa mwaka huu wameweza kusikika kwenye nyimbo za kundi hilo. Bonta amesikika kwenye wimbo uitwao Mdundiko, huku Lord Eyes akitamba kwenye ngoma, Swagire.

Utakumbuka tangu kuundwa kwa kundi hili ni wimbo mmoja tu ambao umeweza kuwakutanisha wasanii wote, wimbo huo unakwenda kwa jina la Watoto wa Mungu.


Mwaka jana walipanda jukwaa moja na rapa kutoka Marekani, Future alipokuja Tanzania. Mwaka huu pia wameweza kushiriki kwenye show kubwa na kufanya vizuri na umekuwa ni utamaduni wao kwa kipindi kirefu sasa.

Kutokana na kufanya kwao vizuri, pia mwaka huu wameendelea kupata mikataba minono ya kuwa mabalozi wa kampuni mbalimbali kwa lengo la kutangaza biashara za kampuni hizo. Ni wasanii wachache sana wanaoweza kupata nafasi kama hizo tena kwa kipindi kirefu kama ilivyo kwao.

Imeandikwa na Peter Akaro