Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amezitaka kampuni za simu za mkononi nchini kurudisha faida kwa jamii ambayo ni wateja wake na wanatumia huduma za mawasiliano za kampuni zao.
Nditiye ameyasema hayo wakati akikabidhi vifaa mbali mbali vya hospitali kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa ikiwemo vitanda, neti, mashuka na aproni vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni sita kwa niaba Serikali kwa Hospitali ya Makole iliyopo Dodoma vilivyotolewa na kampuni ya simu za mkononi ya Halotel
"Nitoe wito kwa kampuni nyingine za simu za mkononi ziige mfano wa Halotel wa kurudisha shukrani kwa wananchi," amesema Nditiye
Pia ameongeza kuwa mawasiliano ni moja ya Sekta ambayo inashika nafasi ya tano kwa maswali Bungeni ikiwemo Sekta nyingine za maji, afya, elimu, umeme, barabara ambapo Wabunge wamekuwa wakiuliza maswali mara kwa mara kuhusu Sekta ya Mawasiliano ambapo inadhihirisha kuwa wananchi wanatambua na kuthamini mchango wa mawasiliano katika maisha yao ya kila siku kwa kuwa mawasiliano ni uchumi na ni maendeleo
Vile vile amezitaka kampuni za simu za mkononi nne zilizosaini mkataba na kupewa ruzuku na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mwezi Disemba mwaka jana ikiwemo Vodacom, TIGO, Halotel na Shirika la Mawasiliano Tanzania kujenga minara ya na kupeleka huduma za mawasiliano haraka kwa wananchi
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Makole, Dodoma Dkt. George Matiko akipokea misaada hiyo ameishukuru kampuni hiyo na kusema kuwa anaipongeza kwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya nchi nzima.