Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe iliyopo Mkoa wa Pwani imeazimia kwa pamoja kupitisha makadirio ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2019 /2020 kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na matumizi mengine.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Hamisi Dikupatile akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani la kupitisha bajeti ya mwaka 2019 /2020 amewataka watendaji wote kuachana kabisa na tabia ya uzembe na badala yake wahakikishe wanajikita zaidi katika kusimamia miradi ya maendeleo pamoja na kuongeza kasi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato kwa maslahi ya Wananchi.
“Kwanza kabisa nipende kuwashukuru madiwani na watendaji wote ambao kwa namna moja au nyingine mmeweza kushirikiana kwa pamoja hadi kuweza kufanikisha mpango huu wa bajeti kwa hiyo kikubwa mimi ninachowaomba tuongeze kasi zaidi katika kukusanya mapato ya ndani ili tuweze kufikia malengo ambayo tumejiwekea,”alisema Dikupatile.
Aidha alisema kwamba lengo kubwa la Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ni kuweka mikakati madhubuti katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kuibua miradi mingine mbali mbali ambayo itaweza kusaidia kwa kiasi kukubwa katika suala zima la kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kibuta Mhandisi Mohamed Kilumbi akizungumza kwa niaba ya wenzake amebainisha kuwa bajeti ambayo wameipitisha itaweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo ikiwemo kumuunga Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli katika kutekeleza azma ya ujenzi wa viwanda.