Mafundi Umeme wote wasio na leseni ya EWURA ya kutoa huduma hiyo kwa Umma wametakiwa na Shirika la Umeme TANESCO Mkoa wa Njombe kukata mara moja leseni hizo ili kudhibiti Mafundi vishoka ambao wamekuwa wakitoa huduma hiyo kinyemela huku ikiwa chini ya kiwango na kusababisha majanga ya moto katika nyumba za wateja wengi Mkoani humo.
Agizo hilo limetolewa na Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Njombe Eng Yusuph Salim katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wakandarasi na mafundi umeme mkoani humo UMAU ambapo amesema shirika limefikia hatua hiyo kufuatia majanga ya nyumba nyingi kuungua na shoti za mara kwa mara ambazo zinasababishwa na dosari za ufundi wa vishoka na kudai kwamba mafundi hao wasio na sifa watadhibitiwa kwa kupitia leseni hizo ambazo zinatolewa kwa kuzingatia vigezo vya EWURA.
Katika mkutano huo pia shirika la tanesco limetakiwa kuongeza idadi ya watumishi na vitendea kazi ili kutekeleza majukumu yao kwa wakati pindi tatizo linapotokea.