Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameziagiza Halmashsuri zote nchini kuhakikisha zinaweka mikakati thabiti ili kutokomeza Magonjwa ya Matende na Mabusha nchini.
Ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi wa kambi ya upasuaji kwa watu wenye tatizo la ugonjwa wa Mabusha na kuangalia hali ya utoaji Huduma za Afya katika Hospitali ya Vijibweni Manispaa ya Kigamboni Mkoa wa Dar es salaam.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa Halmashsuri zote nchini wakati zinaandaa Vipaumbele ni lazima watenge bajeti kwaajili ya mipango endelevu ili kuhakikisha kwamba zinaweza kupambana na Magonjwa haya yaliyokuwa hayapewi kipaumbele bila kuwategemea Wafadhili.
“Niwaombe sana, Wakati mnaandaa Mipango hii, tusiweke masuala mengi ya Semina, tuelekeze nguvu katika intervention, tuweke vitu ambavyo vitaleta mabadiliko, tutenge fedha kwaajili ya mipango endelevu, kwaajili yakuhakikisha kwamba tunaanza kujisimamia katika Magonjwa haya, haipendezi kama nchi kwenda kulia kwa Wafadhili kwa mambo ambayo tunaweza kuyafanya” amesema Dkt. Ndugulile.
Mbali na hayo, Dkt. Ndugulile amesema kuwa, kati ya Wilaya 120 ambazo zilikuwa na uambukizo wa magonjwa haya, Wilaya 96 zimeweza kupunguza maambukizi kwa asilimia 80, hivyo kufikia kiwango cha kusimamisha ugawaji wa Kingatiba kwa jamii katika Wilaya hizo.