F Kenya kuanza kutumia Pikipiki za umeme | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kenya kuanza kutumia Pikipiki za umeme


Kenya itaanza kutumia pikipiki za umeme ndani ya miezi minne ijayo, ukiwa ni mpango wa kukabiliana na foleni barabarani, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kurahisisha usafiri kwa umma.

Akieleza mchakato wa kukamilisha mkakati huo, gavana wa Kisumu, Profesa Anyang’ Nyong'o alisema mara tu alipochaguliwa kuiongoza kaunti hiyo, usafiri wa umma ndio changamoto iliyokuwa inamsumbua kichwa.

Baada ya kutafakari na kukosa majibu ya uhakika, alisema alienda kuomba ushauri ofisi za Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (Unep) ambako alielezwa kuhusu pikipiki za umeme.

"Pikipiki hizi zitapunguza uchafuzi wa mazingira na kelele mjini huku zikiongeza kipato cha madereva ambao hawatonunua tena mafuta," alisema Profesa Nyong'o.

Katika kuhakikisha mkakati huo unatekelezwa kwa mafanikio, Profesa Nyong'o alisema Kaunti ya Kisumu itaweka mazingira yote muhimu kwa wananchi kunufaika nayo.

Kufanikisha usafiri huo wa kisasa, unaolinda mazingira na kujali afya za wananchi, Kisumu inashirikiana na Unep inayoratibu kuenea kwa teknolojia hiyo pamoja na kampuni ya TAILG Group kutoka China inayotengeneza pikipiki hizo.

Meneja mkuu wa TAILG Group, Jayson Huang alisema kuna nchi tatu Afrika Mashariki ambazo zimewekwa kwenye mpango wa majaribio wa matumizi ya pikipiki hizo za umeme. Alizitaja nyingine kuwa ni Uganda na Ethiopia.

"Hii ni teknolojia inayotumika kwa muda mrefu nchini China na maeneo mengine duniani. Si ngeni. Kisumu wataanza kupokea pikipiki ndani ya miezi mitatu au minne ijayo," alisema Huang.

Pikipiki moja, taarifa za matumizi zinaonyesha inaweza kubeba mpaka kilo 150 na ikichajiwa vyema inatembea kati ya kilomita 80 na 100.

Kuhusu uwezekano wa kuzileta  pikipiki hizo nchini, Huang alisema endapo Serikali itaonyesha nia ya kuzihitaji basi iwasiliane na Unep kwa ajili ya kukamilisha masuala ya kimkataba.

Akibainisha faida za pikipiki hizo, mkuu ya idara ya usafi wa anga na usafiri wa Unep, Rob De Jong si tu zitapunguza foleni basi uchafuzi wa mazingira.