Wanunuzi wa sangara katika Halmashauri ya Buchosa, Sengerema mkoani Mwanza, wameilalamikia halmashauri hiyo kuwatoza ushuru wa Sh. 200 kwa kila kilo moja.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanunuzi wa Samaki hao, Gregory Kazimbo juzi alisema kuwa ushuru huo ni mkubwa kwa sababu kwenye mialo wanalazimika kununua kwa Sh. 3,500 kwa kilo na kuuza viwandani kwa Sh. 4,000.
"Tumepeleka maombi yetu katika halmashauri hiyo ili Baraza la Madiwani litusaidie kubadilisha ushuru huo mkubwa kwa kila kilo ya samaki Sh. 200. Tunaomba iwe angalau Sh. 30,” alisema Kazimbo.
Kazimbo alisema umoja huo ulianzishwa kutoka katika mialo ya Mkoamani, Nyakaliro, Nyarusenyi, Ntama, Mchangani, Mbugani, Kanyara, Chembaya, Kabiga na Kahunda.
Alisema awali walikuwa wakilipa ushuru wa jumla kwa kila tripu moja ambayo ilikuwa Sh. 100,000 lakini sasa umebadilika jambo ambalo linawaumiza katika biashara hiyo na kuwakosesha faida.
Hata hivyo alisema wanaiomba halmashauri kuendelea kuwatoza ushuru wa jumla wa Sh. 150,000 badala ya sasa ambao unawaumiza.