F Wafugaji watakiwa kuchangamkia chanjo ya mifugo | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wafugaji watakiwa kuchangamkia chanjo ya mifugo


Na. Ahmad Mmow,Nachingwea

Wafugaji wilayani Kilwa mkoa wa Lindi wametakiwa kushiriki kikamilifu zoezi la chanjo ya mifugo yao ili isikumbwe na homa ya mapafu.

Agizo hilo limetolewa leo na mkuu wa wilaya ya Kilwa,Christopher Ngubiagai alipozungumza na Muungwana Blog kutoka Kilwa Masoko,ambako yapo makao makuu ya wilaya hiyo.

Ngubiagai amewataka wafugaji wote kushiriki zoezi hilo ambalo lilitarajiwa kuanza leo.Huku akisisitiza kwamba gharama ya kuchangia kwa ajili ya chanjo hiyo ni ndogo ambayo wafugaji wanaweza kumudu.Kwani wanatakiwa kuchangia shilingi 1,000 tu.

Alisema wafugaji hawanabudi kushiriki kikamilifu zoezi hilo ambalo litafanywa na maofisa wa idara ya mifugo ili kukinga mifugo yao isikumbwe na homa ya mapafu.Huku akiweka wazi kwamba chanjo hiyo itafanyika kwenye maboma(mazizi)ya wafugaji.

Ngubiagai ambae wilaya yake inakadiriwa kuwa na mifugo 57,000,alisema wafugaji hawanabudi  kuunga mkono nia njema ya serikali katika kukinga mifugo yao isipatwe na ugonjwa huo unaoambukiza.

"Serikali inathamini umuhimu wa mifugo na wafugaji katika kukuza uchumi wa nchi na wao wenyewe.Kwahiyo sioni sababu ya mfugajj kushindwa kuchanja mifugo yake.Kwakuwa ni ugonjwa unaoambukiza,basi hili ni agizo,sio suala la hiyari,"alisema Ngubiagai.

Aidha Ngubiagai amewataka viongozi wa vijijji kutoa ushirikiano unaostahili kwa maofisa mifugo na timu iliyoundwa na wilaya hiyo kufanikisha zoezi hilo pindi itakapofika katika vijiji vyao.

Mbali na wafugaji waliopo katika wilaya ya Kilwa,mkuu huyo wa wilaya ametoa wito kwa wafugaji walio nje ya wilaya hiyo na wafanyabiashara wa mifugo wahajikikishe mifugo wanayotaka kuingiza au kupitisha wilaya humo iwe imechanjwa.

Alisema hakuna mfugaji wala mfanyabiashara atayeruhusiwa kuingiza au kupitisha mifugo isiyochanjwa.Badala yake itarejeshwa ilikotoka.Huku akiwataka walinzi waliopo katika vizuizi wahakikishe wanakagua mifugo yote itayoingizwa au kupitishwa.

Hata hivyo Ngubiagai hakusita kuwapongeza wafugaji kwa mwitikio mzuri walioonesha kabla ya zoezi hilo kuanza.Alisema wafugaji wengi wamepokea vizuri taarifa na wito wa serikali kuhusiana na zoezi hilo.Hali inayompa matumaini kwamba litafanikiwa kama inavyokusudiwa.