Na. John Walter,Babati
Mbunge wa Babati Vijijini mkoa wa Manyara Jitu Soni (CCM) amewataka wananchi wa Kijiji cha Guse, Kata ya Bashnet Wilayani Babati Mkoani Manyara kulima zao la biashara la pareto ili kujikomboa katika umasikini .
Alisema kwa kuwa kijiji hicho kipo ukanda wa baridi na ukanda huo hauwezi kuzalisha mazao mengine ya biashara ya mbaazi na alizeti yanayozalishwa kwa wingi Wilayani humo hivyo wanapaswa kupanua mashamba yao kutoka mashamba madogo kuja mashamba makubwa kwa kulima zao la biashara la Pareto.
Akizungumza na wananchi hao kupitia mkutano aliouitisha Mbunge huyo wa jimbo la Babati Vijijini Jitu Son, Kwa mujibu wake Pareto kama zao la biashara linalostawi katika eneo la ukanda wa baridi litawasaidia wananchi hao kuondokana na mazoea ya kulima mahindi na viazi pakee kwa ajili ya mazao ya kujikimu.
Alibainisha kuwa kilimo cha pareto kitachangia pia uchumi wa viwanda kwani kutakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa ajira kwa vijana, akina mama watakajipatia kipato cha kujikimu katika maisha yao na kuwapa elimu watoto wao.
“Hili ni zao zuri kwa ajili ya biashara ikishaanza kutoa maua inavunwa kila baada ya wiki mbili, vijana na kinamama mnaweza kujiunga katika vikundi mkatafuta mikopo na kukodisha shamba ili mlime Pareto kwa kujipatia kipato kwa urahisi zaidi na itawasaidia katika kusomesha, na matumizi ya haraka mkaacha kutegemea mahindi na viazi ” alisema Jitu.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Pareto Tanzania ya Pyrethum Company of Tanzania Ltd (PCT) yenye makao yake Iringa na inayojishughulisha na kununua Pareto nchini imewahakikishia wananchi wa Kijiji cha Guse, kuwa itanunua pareto yote itakayolimwa katika msimu wa mwaka 2019/2020.
Mkurugenzi huyo John Power alisema kampuni hiyo ipo tayari kununua pareto yote itakayozalishwa kwa ubora kwa shilingi 2300 hadi 3000 kwa kilo moja.
John Power aliwataka wananchi hao kuendelea kulima kwa wingi zao hilo na kwamba Kampuni hiyo ina uhitaji mkubwa wa Pareto na inaweza kununua kiasi chochote kitakacholimwa.
“Endeleeni kulima hata kama ni shamba dogo kadri mnavyozidi kupata faida ndio mtaongeza mashamba , sisi tunawahakikishia uhakika wa soko, hatujawahi kufeli kununua hata kilo moja ya pareto kutoka kwa mkulima” alisema Power.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Guse John Gwandu alisema wananchi wameanza kulima kwa wingi baada ya kuona manufaa kwa wachache walioanza kulima zao hilo kwani maisha yao yalibadilika na waliweza kulipa hata michango ya kijiji kwa haraka kwakuwa waliuza pareto., tofauti na zamani ambapo walitegemea viazi tu.
“Wananchi wamepata hamasa ya kulima zao hili kwasababu wale walioanza walipata mafanikio, wengine wanaendelea kuongeza mashamba kila siku, sasa hivi miche mingi ipo kwenye bustani wananchi wengi wanaendelea kuongeza mashamba ili kuongeza pato lao” alisema Gwandu.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Getabuske kijiji cha Guse Baltazari Petro alibainisha kuwa kwa mara ya kwanza zao hilo limeanza kulimwa mwaka huu na wananchi wengi wameitikia wito wa kupanua mashamba yao ingawa changamoto iko katika upatikanaji wa miche.
Kupitia wakala wa ukusanyaji wa pareto kijijini hapo alibainisha kuwa wakulima wengi wamekuwa wakipeleka mazao yao katika kituo cha wakala huyo na kulipwa fedha zao kulingana na ujazo unaotakiwa pasipokuwa na usumbufu wowote.
“Kwa mwaka tunalima misimu miwili ya miezi mitatu, mwaka jana ni wakulima kumi tu walilima Pareto kwa kiwango kidogo baada ya kuona uhakika wa soko wengi wamepanua mashamba yao” alisema Petro.
Katika mkutano huo Mbunge huyo alitoa mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho na Mkurugenzi wa kampuni ya Pareto Tanzania alitoa mifuko 10 ya saruji kama sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya kijiji hicho.