Utangulizi
Leo nimekuandalia makala hii ya kilimo cha mihogo. Kutokana na sifa yake ya kuvumilia ukame kipindi hiki ni muafaka kabisa kwa maandalizi na upembuzi juu ya kilimo cha mihogo kwa msimu ujao wa mvua za vuli. Natumai katika makala hii utajifunza mambo yote muhimu unayohitaji kujua kuhusu muhogo. Karibu…
Zao la muhogo ni muhimu sana kwa Tanzania, zaidi kwa wakulima wadogo wenye kipato cha chini. Wakulima wengi huchanganya mihogo na mazao mengine kama vile kunde, mbaazi, njugumawe, n.k.
Umuhimu wa zao hili ni kutupatia chakula na wakati mwingine kwa biashara. Kwa kanda ya kusini mihogo ni chakula kikuu ambacho kinachuku asilimia 75 ya chakula kwa maeneo yote ya mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kwa siku za karibuni, muhogo unaongoza kwa kuongezeka katika umaarufu kuliko mazao yote ya chakula nchini. Watalaam wanazungumzia umaarufu wa muhogo kuwa ni (pamoja na mambo mengine) uwezo wake wa kustahamili hali ya hewambaya kama ukame na mvua zisizoaminika, kutoa mazao mengi kwa eneo na kustahamili mashambulizi ya magonjwa na wadudu.
Hata hivyo uzalishaji wa mihogo kwa eneo bado ni wa viwango vya chini mno. Zipo sababu nyingi zinazo sababisha kuwepo kwa hali hii kama vile:
- Ukosefu wa mbegu bora za mihogo za kutosha
- Wakulima kuendelea kungangania mbegu zao za asili kuliko mbegu bora licha ya uzalishaji mdogo na kushambuliwa na magonjwa na wadudu.
- Ukosefu wa masoko ya kuaminika ambayo yangeshawishi wakulima kulima mbegu za kisasa ambazo zimeandaliwa kibiashara.
- Wakulima wengi kutotumia teknolojia sahihi za usindikaji ambazo ni mbinu mbadala za hifadhi za asili.
Kwa muda mrefu tatizo kubwa la zao la muhogo ni ukosefu wa teknolojia ambazo zina uwezo wa kuongeza thamani wa muhogo kama chakula chenye ubora kwa familia za mijini na vijijini.
Vikundi mbalimbali vya uzalishaji na usindikaji vimeundwa na muhogo umeanza kuthaminwa kwani unga wake unatumika kutengenezea vyakula kama maandazi, chapati, chichili, keki na vingenevyo vingi.
Ugali wa muhogo umeongezeka thamani kutokana na ubora wa unga uliosindikwa kwa kwa teknolojia ya kisasa.
Madhumuni ya Mogriculture Tz kutoa makala hii ni kutoa maelekezo juu kilimo bora cha zao la muhogo ili kusaidia wakulima kuinua viwango vya ubora na wingi wa mazao hivyo kujihakikishia usalama wa chakula na kujiongezea kipato.
Umuhimu na Matumizi ya Muhogo
- Muhogo ama (kitaalam) Manihot esculentum, ni muhimu sana kwa Tanzania kutokana na sifa zake za kuvumilia ukame, kustawi kwenye maeneo yenye rutuba kidogo hivyo kuhitaji gharama ndogo za uzalishaji. Kwa hali hiyo, zao hili hulimwa sana na wakulima wadogo walio wengi wenye kipato kidogo.
- Kwa wakazi wa vijijini, muhogo huvunwa, kutolewa ganda la juu na kuanikwa hadi kukauka maarufu kama makopa. Kwa kawaida makopa hutwangwa kwenye kinu na kupata unga ambao hutumika kama uji au ugali. Makopa mara nyingi hutunwa ama kuhifadhiwa kwenye dari ya nyumba ambako hufukiziwa moshi wa moto ili yasipukuswe.
- Kutokana na hali hiyo, wakulima wengi hulima muhogo mchungu ambao haupukuswi kwa urahisi. Kwa vile muhogo mchungu una sumu nyingi aina ya cyanide, hufanya kiasi kidogo cha muhogo kiliwe kwa kutafuna ukiwa mbichi ama kupikwa kama futari.
- Kwa wakazi wa mijini, sehemu kubwa ya mihogo hutumika kama futari au kitafunwa kwa chai ama humenywa na kukaangwa kama chips maarufu kama chips dume.
- Kutokana na kuongezeka kwa teknolojia za usindikaji, unga wa muhogo hutumika kutengenezea biskuti, chapati,maandazi,chichili,keki na vyakula vingine vingi vinavyotengenezwa kwa kutumia unga wa ngano.
Mazingira na Aina za Mihogo
Mazingira yanayofaa
Muhogo ni zao la jamii ya mizizi. Hustawi vizuri katika maeneo yaliyopo kwenye mwinuko wa mita 0 hadi 1500 toka usawa wa bahari. Zao hili hustawi vizuri kwenye maeneo yanayopata mvua ya wastani wa milimita 750 mpaka milimita 1200 kwa mwaka.
Muhogo hupendelea udongo wa kichanga usiotuamisha maji. Udongo wa kichanga husaidia mizizi kupenya kwa urahisi na kupevuka. Vile vile muhogo una sifa ya kuvumilia hali ya ukame wa muda mrefu.
Aina za Mihogo
Kuna zaidi ya aina 45 za mihogo zinajulikana nchini Tanzania. Zaidi ya asilimia 80 ya mihogo ni ya asili. Hivyo ni kusema wakulima wengi hawatumii mbegu bora.
Wakulima wengi pia hupendelea kulima mihogo michungu kwa sababu haishambuliwi sana na wadudu ama magonjwa shambani na makopa yake yanahifadhika kwa urahisi. Hata hivyo zaidi ya asilimia 70 ya mihogo yote inayolimwa Tanzania ni mihogo baridi.
Kuandaa shamba la Muhogo
Inashauriwa kuandaa shamba mapema kabla ya msimu wa mvua haujaanza. Zifuatazo ni hatua za msingi katika kuandaa shamba:
- Kufyeka msitu au vichaka
- Kung’oa na kuchoma moto visiki
- kulima na kutengeneza matuta.
Uchaguzi wa mbegu bora za mihogo
Mpaka sasa hivi kuna aina nyingi sana za mbegu bora za mihogo ambazo zimethibitishwa na tayari zinatumiwa na wakulima. Mbegu hizi huvumilia magonjwa (batobato na matekenya), pia huzaa sana ukilinganisha na mbegu za kienyeji.
Katika kuchagua mbegu inayofaa, pamoja na mambo mengine, zingatia yafuatayo:
- Mbegu itokane na shina lililokomaa vizuri
- Isitokane na shina la muhogo ulioshambuliwa na magonjwa.
- Macho yake yasiwe yamekaribiana sana au kuachana sana
Upandaji wa Mihogo
Muda wa kupanda Mihogo
- Kanda ya ziwa: December mpaka January mwishoni
- Nyanda za juu Kusini: November mwanzoni na Kanda ya Mashariki: kuanzia October mpaka December
Urefu wa kipande cha shina cha muhogo
Baada ya kuchagua mbegu hatua inayofuata ni kukata shina lako la muhogo katika pingili ndogo ndogo tayari kwa kupanda. Inapendekezwa pingili ziwe na urefu wa sentimita 30.
Hata hivyo, urefu wa pingili utategemea sana idadi ya macho yaliyopo kwenye hicho kipande. Inapendekezwa kipande kimoja kiwe na macho manne hadi sita.
Nafasi ya kupanda Muhogo
Nafasi ya kupanda kwa shamba linalokusudiwa liwe na muhogo mtupu ni mita moja toka shina hadi shina na mita moja kati ya mistari. Kwa shamba ambalo mkulima anakusudia kuchanganya mazao, inashauriwa nafasi ya kupanda iwe mita 2 hadi mita 4 (kwa kutegemea aina ya mazao yanayochanganywa) kati ya mistari na mita moja toka shina hadi shina.
Kuna njia tatu za upandaji wa muhogo:
- Kulaza ardhini (Horizontal)
- Kusimamisha wima (Vertical) na
- Kuinamisha ( Inclined/Slunted)
Kudhibiti Magugu
Katika miezi minne ya mwanzo muhogo unahitaji kupata chakula cha kutosha na mahitaji mengine ya msingi ili uweze kukua na kujenga mizizi mikubwa na imara. Hivyo inashauriwa kufanya palizi la kwanza mapema, angalau mwezi mmoja baada ya kupanda ili kuepukana na magugu yanayochipua haraka baada ya mvua za mwanzo kunyesha.
Kwa kawaida palizi hufanywa kwa kutumia jembe la mkono au dawa ya kuulia magugu. Njia nyingine ya kudhibiti magugu ni kupanda mimea yenye majani yanayotanda juu ya udongo.
Palizi kwa kawaida hufanywa kila inapoonekana kwamba magugu yameota kiasi cha kuathiri ustawi wa muhogo, hivyo unaweza kupalilia mara 3 au 4 zaidi baada ya palizi ya kwanza hadi muhogo kukomaa.
Kuchanganya mazao kwenye shamba la mihogo
Utafiti unaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya mashamba ya muhogo Tanzania yanachanganywa na mazao mengine. Sababu kubwa zinazotolewa kuhusiana na hali ni kwamba wakulima wanafaidika kwa kupata mavuno ya ziada kama kunde, karanga, mahindi, maharage, korosho ama njugu.
Kwa kuchanganya mazao, mkulima, licha ya kuimarisha uhakika na usalama wa chakula, anaweza kuuza mazao mchanganyiko na kujiongezea kipato. Vile vile mazao ya jamii ya mikunde yanasaidia kuongeza rutuba ya udongo.
Hata hivyo, mazao mchanganyiko ni budi yasilete ushindani na muhogo katika kujipatia chakula, hewa, mwanga, unyevu na mahitaji mengine ya mmea yanayoweza kuathiri ustawi wa muhogo.
Inashauriwa pia kuzingatia muda wa kupanda, yaani muhogo upandwe mvua za kwanza ili mazao mchanganyiko yasiweze kuzidi na kuutawala muhogo.
Jinsi ya kudhibiti Wadudu na Magonjwa
- Aina Bora za Mbegu za Mihogo
- Wadudu na Magonjwa ya zao la Muhogo
- Jinsi ya kufanya Kilimo Bora cha Karoti
Uvunaji wa Muhogo
Mihogo inaweza kuanza kuvunwa baada ya miezi 9 – 12 tangu kupandwa. Inashauriwa kuvuna katika katika kipindi cha jua; kwani wakati wa mvua kiwango cha wanga kwenye muhogo hupungua. Mihogo hutoa mavuno ya tani 19 hadi 30 kwa hekta kutegemeana na aina ya mbegu (variety) iliyopandwa.
Usindikaji bora wa Muhogo
Usindikaji bora wa muhogo unafanyika kwa sababu kuu tatu:
- Kurahisisha/kuharakisha ukaushaji
- Kuondoa sumu (cyanide) ilyoko kwenye baadhi ya aina za mihogo
- Kuongeza ubora wa unga utokanao muhogo wenyewe.
Njia bora za usindikaji Muhogo
- Kwa kutumia mashine aina ya Grater
Hii hutoa chembechembe laini za muhogo, ambazo baadae hukamuliwa kwa kutumia kifaa kingine kiitwacho “presser” ili kuondo sumu iliyoko kwenye muhogo. Mashine hii hutumika hususani kwa muhogo mchungu.
- Kwa kutumia mashine aina ya chipper
Mashine hii hutoa vipande vidogo vidogo (chips). Mashine hii hutumika hasa hasa kwa ajili ya mihogo mitamu/baridi.
Matumizi ya Muhogo
- Muhogo unaweza kupikwa wenyewe kama chakula au kutengeneza unga
- Unga wa muhogo unaweza kutengeneza vitu vyotekama vinavyotengenezwa na unga wa ngano kama vile biskuti, chapatti, maandazi, chichili, keki n.k.
- Pia muhogo huweza kutumika viwandani kutengeneza bidhaa nyingine kama vile wanga.
Ni matumaini yangu kuwa umejifunza mambo mengi mazuri kuhusu kilimo cha muhogo, sasa tumia angalau dakika mbili tu kutupatia mrejesho kwa kuandika comment yako hapa chini.