Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amezitaka halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika utoaji wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye walemavu.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya zaidi ya shilingi bil 1.06 (1,062,500,000) kutoka katika mapato ya ndani ya Jiji laDodoma kwa mwaka wa Fedha 2018/19 kwa vikundi 201.
Alisema kuwa halmashauri zingine zihakikishe kuwa asilimia 10 ya mapato yao ya ndani inapelekwa moja kwa moja kwenye vikundi vya wanawake na vijana na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi.
“ Jiji la Dodoma limekuwa la mfano katika mambo mengi kuanzia ukusanyaji wa mapato wameongoza katika pato ghafi na leo hii wametekeleza kwa vitendo Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura Na, 290 kifungu 37A na kanuni zake za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi
vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019.
Jafo aliongeza: “ Kukusanya mapato ni jambo moja na utoai wa mikopo ni jambo jingine, halmashauri inaweza kukusanya lakini isitoe mikopo hii kwa vikundi, sasa Dodoma wameyafanya yote haya kwa umakini na ufanisi mkubwa niwapongeze Jiji la Dodoma na niwatake
Halmashauri zingine waje kujifunza na kuiga mfano wenu mnafanya kazi nzuri.