F Halmashauri ya Rorya yabuni mradi wa Kilimo cha Pamba | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Halmashauri ya Rorya yabuni mradi wa Kilimo cha Pamba


Na.Timothy Itembe Mara

Mkuu wa wilaya Rorya, Saimon Chacha amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kwenda katika maeneo yao na kuhamasisha Wananchi kuchangamkia kilimo cha Pamba kilichombioni kuanza ili kujipatia kipato na kukuza mapato ya halmashauri.

"Niwaombe ndugu zangu madiwani mliochaguliwa na wananchi katika maeneo yenu kwenda na kuhamasisha kilimo cha Pamba ili halmashauri yetu ikapate mapato pamoja na wakulima kunufaika na kilimo cha pamba kwa kuwa zao la Pamba ni moja ya mazao yaliyopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli"alisema Chacha.

Chacha alitaja mazao hayo ambayo yamepewa kipaumbele na serikali ya awamu ya Tano kuwa ni Pamba,Chai,Kahawa,Korosho na Tumbaku na kuwa ili kujenga Tanzania mpya ya viwanda kuna kila sababu wananchi na viongozi kutekeleza sera ya serikali ya wamu ya Tano.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Charles Chacha alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 halmashauri yake imeweza kuongeza mapato shilingi Milion 595 kutoka shilingi milion 530 ambayo ni makusanyo ya mwaka wa fedha 2015/2016.

Chacha aliwataka madiwani pamoja na wananchi kuunga juhudi za halmashauri yake katika jukumu zima la kukusanya mapato ili halmashauri hiyo ibaki na kazi ya kutekeleza miradi iiyokusudiwa kwa wananchi wake.

Naye Diwani kata ya Kitembe Chadema alisema kuwa halmashauri yake inavyanzo kiduchu vya mapato kwa hali hiyo kuna haja halmashauri kujipanga na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza makusanyo katika halmashauri hiyo na kuwa rahisi kuwatekelezea wananchi miradi siovinginevyo.