Mkurugenzi wa kampuni ya Candy N' Candy ya nchini Kenya na wazalishaji wa jarida la Babkubwa hapa Tanzania, Joe Kariuki ameushukuru uongozi wa serikali ya awamu ya tano unaoongozwa na Dkt. John Magufuli kwa kutenda haki hadi kuachiliwa huru kutokana na kesi aliyokuwa anatuhumiwa ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Joe amesema hayo wakati akifanya mahojiano na vyombo vya habari akiwa jijini Nairobi, Kenya ambapo amesema anaishukuru mahakama ya Arusha kwa kutenda haki hadi kuachiliwa huru ambapo aliweza kukaa gerezani kwa takribani mwaka mmoja tangu alipohukumiwa kwenda jela miaka saba na kisha kushinda rufaa yake.
"Kwa kweli naishukuru mahakama ya Arusha kwa kuweza kutenda haki hadi mimi kuachiliwa huru kwa kushinda rufaa hii imedhihirisha kwamba serikali hii ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imekuwa ikisimamia haki katika vyombo vyake kwa kusikilizwa kesi kwa haraka zaidi na kutenda haki" amesema Joe Kariuki.
Pia ameongeza kwa kuwashukuru Watanzania wote na wafanyakazi aliokuwa akifanya nao kazi kipindi akiwa Tanzania na kusema muda si mrefu angependa kurudi tena na kuendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali na kutoa ajira kwa watanzania.
"Nipende kuwashukuru watu niliokuwa nikifanya nao kazi na watanzaia wote kwa kuniombea na kuwa pamoja na mimi katika kipindi hiki kigumu nilichopitia, nawaahidi ningependa kurudi Tanzania na kuendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali hivyo bado tupo pamoja."
Joe Kariuki alikamatwa Namanga wilaya ya Longido mnamo Julai 2, 2018 na kufikishwa katika mahakama ya wilaya ya Longido na kufunguliwa mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mfanyabiashara mwenzake Yusuf Mohamed, na kuhukumiwa kwenda jela miaka saba kabla ya kushinda rufaa yake na kuachiliwa huru Mei 10 ya mwaka huu na mahakama ya Arusha.