F Namanga kufanyika kipimo cha tahadhari ya ebola | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Namanga kufanyika kipimo cha tahadhari ya ebola


Kipimo cha tahadhari cha ugonjwa wa ebola kinatarajia kufanyika katika mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Namanga kwa muda wa siku nne kuanzia Juni 11, mwaka huu.

Daktari Michael Katende, kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki Idara ya Afya, aliwataka wananchi kutoogopa tukio hilo kwa sababu lengo lake ni kuhakikisha nchi zinakuwa kwenye usalama wa magonjwa ya milipuko.

Dk. Katende alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na chombo kimoja cha habari kuhusu utekelezaji huo utakaoanza Juni 11 hadi 14, mwaka huu, katika mpaka wa Namanga na kuhusisha nchi za Tanzania na Kenya.

"Lengo ni kujua namna nchi zetu zilivyojipanga kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwamo ebola," alisema.

Alisema wanafahamu kuwa kila nchi ina mikakati yake ya kukabiliana na magonjwa, lakini kitakachofanyika siku hiyo ni kuongeza uelewa zaidi pamoja na kuangalia changamoto ambazo zinahitaji ufumbuzi kabla ya magonjwa kujitokeza.

"Unawaomba watu wanaosafiri na kupita mpaka wa Namanda wasiwe na wasiwasi siku hiyo kwa sababu tunachokifanya ni kujua nguvu yetu ya kukabiliana na magonjwa na changamoto zake," alisisitiza.

Alisema siku hiyo wanatarajia kuwa na watu 250 na huduma hiyo itatolewa kwa nchi hizo.

Pia alisema watakuwa na wageni kutoka nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki na wageni wengine wa mataifa mbalimbali duniani.

"Tunataka tuwe na uhakika nchi zetu tupoje katika kukabiliana na ebola, je, tumejiandaa kwa kiwango gani? Maeneo gani au vitu gani tunatakiwa kuongeza nguvu. Tunatarajia kupata mrejesho ili kujua nini kinatakiwa kufanyika," alisema.

Ugonjwa wa ebola husababishwa na virusi vya ebola ambavyo huambukiza kwa njia zifuatazo; kugusa damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo. Kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo. Kugusa wanyama (mizoga na wanyama wazima) walioambukizwa kama vile sokwe na swala wa msituni.

Wakati mtu anapoambukizwa hadi dalili za ugonjwa huo zinapoanza kuonekana ni kati ya siku mbili hadi 21 na mara nyingi dalili huanza kuonekana kati ya siku ya nane hadi ya kumi baada ya kuambukizwa, zikijidhihirisha kama dalili za malaria au homa.

Dalili za ebola zinatajwa kuwa ni pamoja na homa, kichefuchefu na kutapika, kuharisha, vidonda vya koo, kuumwa kichwa, maumivu ya misuli, kusumbuliwa na tumbo, kuchoka, kukosa hamu ya kula ambazo zinaweza kujitokeza zote kwa pamoja, ingawa mgonjwa anaweza kuwa na dalili moja au mbili kati ya hizo.

Dalili hizo huweza kujitokeza siku ya tano baada ya mtu kuona dalili za kwanza za ugonjwa huo na anaweza kutokwa na damu kupitia tundu za mwili kama mdomoni, puani na sehemu za siri.

Baada ya kupatikana na virusi vya ebola, mgonjwa anapaswa kujitenga na wengine, mfano asisalimiane kwa mikono, kumbusu mwengine au kufanya tendo la ngono.

Sampuli za damu, mate na mkojo lazima zipelekwe maabara yenye vifaa vya kuaminika ili kufanyiwa uchunguzi wa kina kubainisha mapema virusi hivyo.

Mwaka jana, Shirika la Afya Duniani (WHO), lilizitaka Uganda, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi zichukue tahadhari ya haraka kutokana na kusambaa kwa ugonjwa huo.

Shirika hilo lilisema hatari ni kubwa kwa Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini na tayari nchi hizo zimeambiwa kuchukuwa hatua za haraka ili kuzuia ugonjwa huo.

WHO ilitoa kauli hiyo baada ya mkutano maalumu wa dharura uliofanyika mjini Geneva kujadili hali ya ugonjwa huu nchini ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako takwimu zilionyesha kati ya watu 10 walioambukizwa ebola sita hufariki.

Agosti 11, mwaka jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema Tanzania hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya ebola.