Wanafunzi, Innocent Shirima na Sada Kimangale kutoka shule za Sekondari Moshi (Kilimanjaro) na shule ya Sekondari Kwemnabara (Tanga) wameshinda nafasi ya kwanza ya uandishi wa insha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa mwaka 2018.
Wanafunzi hao wamepewa vyeti na zawadi kwa ngazi ya kitaifa, leo Jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu.
Akitoa hotuba wakati wa utoaji wa vyeti kwa wanafunzi hao, Dkt. Semakafu amesema Watanzania waache kujizalilisha kwa kusema shule za Serikali sio bora, kwani watoto hao wanaozalilishwa wakienda kwenye ngazi ya Kimataifa wanafanya vizuri.
“Tukio la leo linatuma ujumbe kwa wale wote wanaoiponda elimu ya Tanzania, kwani washidi wa kwanza wa insha za EAC na SADC wote wanatoka katika shule za Serikali ambazo zinapondwa kila siku,” amesema Dkt. Semakafu.
Ameeleza kuwa, walioifikisha Tanzania hapa ilipo ni Watanzania waliosoma hapahapa Tanzania na wala sio watu waliosoma nje ya Tanzania.
Aidha amempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufungua na kupaanua wigo wa elimu kwa Serikali kulipa gharama za wanafunzi hivyo kuwezesha watoto wote wa Tanzania kupata fursa kupata elimu.
Kwa upande wake, Mratibu wa mashindano hayo kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Sylivia Chinguwile amesema mashindano ya uandishi wa insha yamekuwa chachu kwa vijana kufanya utafiti, kujifunza na kufahamu vizuri mchakato na hatua mbalimbali za uimarishaji mahusiano kwa nchi wanachama.
Naye, Mshindi wa Insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Innocent Shirima ambaye pia ni mlemavu wa macho, amesema mashindano yamewapa fursa ya kujifunza masuala ya jumuiya hiyo.
 |
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Moshi ya Watu wenye mahitaji maalum, Innocent Shirima Akitoa neon la shukrani kwa niaba ya wenzake wakati wa hafla fupi ya kutoa zawadi kwa wanafunzi walioshinda mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma |