F Uhaba wa mchanga Zanzibar, Balozi Seif atoa agizo kwa Wizara | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Uhaba wa mchanga Zanzibar, Balozi Seif atoa agizo kwa Wizara



Na Thabit Hamidu,Zanzibar.

Licha ya kuwepo kwa  uhaba wa Mchanga ndani ya visiwa vya Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa  Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi pamoja na Kamati Maalum inayosimamia Rasilmali ya Mchanga kutoa kibali cha upatikanaji wa Mchanga kwa Miradi mikubwa ya Serikali ili kuepusha mkwamo wa utekelezaji wa Miradi hiyo.

Amesema haitopendeza  ifike wakati miradi ikwame kisa kutopatikana kwa mchanga.

Aidha amesema hatoridhika kufika wakati wanyoosheane vidole na Wahandisi wa Makampuni ya Ujenzi wa Miradi Mikubwa kwa madai ya kuchelewesha kazi waliyopewa wakati.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo  jana wakati  wakati wa ziara ya kutembelea ujenzi wa miundombinu ya Madaraja, Mitaro ya Maji ya Mvua, kukagua maeneo yaliyoathirika na mafuriko ya Mvua za Masika zinazoendelea pamoja na kuwafariji Wananchi waliopatwa na athari hizo ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema upo Urasimu unaofanywa na baadhi ya wasimamizi wa utoaji wa Vibali vya Rasilmali ya Mchanga jambo ambalo zipo dalili zinazoanza kuonekana za kuchelewa kukamilika kwa baadhi ya Miradi ambayo ni muhimu kwa Taifa na Wananchi.

Balozi aliongeza kusema kazi kubwa iliyofanywa na Wahandisi wa Makampuni yanayojenga Madaraja ya Kibonde Mzungu na Mwanakwerekwe imeleta faraja kubwa kwa Taifa na Wananchi waliowengi hapa Nchini.


Pia  alisema changamoto ya kujaa kwa maji katika madaraja hayo inaanza kuwa Historia kwa vile licha ya kutokukamilika rasmi kwa Ujenzi wake lakini Wananchi wapitao kwenye Madaraja hayo hivi sasa wanaendelea na harakati zao kama kawaida katika maeneo ambayo ilikuwa mwiko kupita katika kipindi hichi.

Akitoa pole kwa Wananchi waliokumbwa na mafuriko kutokana na Makaazi yao kujaa maji katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Kwamtumwa Jeni, Sebleni na Jong’ombe, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliwanasihi baadhi ya Wananchi kuwa na Utamaduni wa kutupa taka katika sehemu Maalum zilizotengwa.

Alisema Serikali imekuwa ikichukuwa jitihada kubwa za kujenga miundombinu ya Mitaro ya Maji ya Mvua lakini wapo Watu wasiozingatia jitihada hizo jambo ambalo linarejesha nyuma utekelezaji wa mipango ya kuwahudumia katika kuimarisha ustawi wao.


Hata hivyo Balozi Seif aliwataka Wananchi wa maeneo yanayopitishwa ujenzi wa Mitaro mipya ya Maji ya Mvua kuwa na subira katika kipindi hichi cha mpito cha Ujenzi unaoendelea kwa vile ukamilikaji wa miradi hiyo utaleta faraja ya kudumu hapo baadae.