Mbegu za nyanya huoteshwa kwanza kwenye kitalu na baadaye huhamishiwa shambani. Matayarisho ya kitalu hufanyika wiki 1 au 2 kabla ya kusia mbegu. Tengeneza tuta lenye upana wa mita 1 na urefu wa kuanzia mita 5 hadi urefu unaoweza kuhudumia kwa urahisi. Vunja mabonge makubwa kwa kutumia jembena kulainisha udongo vizuri.Changanya mbolea za asili zilizooza vizuri kama vile Samadi au mboji kiasi cha debe 1- 2 katika eneo la mita mraba 1.
Sawazisha kwa kutumia reki au kifaa kingine. Mwagilia kitalu siku moja kabla ya kusia, kisha sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 10 – 15 kutoka mstari hadi mstari.
Kiasi kinachotosha eneo la mita mraba 1 ni gramu 3 – 5 (sawa na nusu kijiko cha chai hadi kimoja) Kiasi hiki cha mbegu huweza kutoa miche inayoweza kutosha kupandikiza katika eneo la mita mraba 100. Kiasi cha mbegu kinachohitajika kwa hekta 1 ni gramu 300.
Weka matandazo kama vile nyasi kavu na kasha mwagilia maji asubuhi na jioni mpaka mbegu zitakapoota.Mbegu huota baada ya siku 5 – 10. Ondoa matandazo baada ya mbegu kuota na endelea kumwagilia maji hadi miche itakapofikia kupandikizwa.Jenga kichanja ili kzuia jua kali na matone ya mvua yasiweze kuharibu miche michanga.