Ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira, mdau wa mazingira ameanzisha kiwanda cha kutengeneza mkaa mbadala wilayani Bunda, ambao utauzwa kwa bei nafuu kwa watumiaji.
Kiwanda hicho, Charcoal Investments kitasaidia kukabili uharibifu wa mazingira.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Eliphas Mollel, mkazi wa wilayani Bunda alisema aliamua kuanzisha kiwanda hicho kidogo cha kutengeneza mkaa mbadala ili kuwawezesha wananchi kuacha tabia ya kukata miti kwa matumizi ya binadamu.
Kiwanda hicho kiko Bunda Stoo Halmashauri ya Mji wa Bunda, kitakuwa kinatengeneza mkaa mbadala kwa malighafi za kawaida, takataka zinazopatikana katika mazingira ya jamii.
Mollel alisema uharibifu wa mazingira kwa kukata miti kuchoma mkaa ni mkubwa Bunda.
Alisema ameanzisha kiwanda hicho kutunza na kuhifadhi mazingira, kutoa ajira kwa vijana akiunga mkono kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya serikali ya viwanda kuelekea uchumi wa kati na kutoa ajira kwa Watanzania.
Mollel alisema kiwanda hicho kitapunguza changamoto hiyo ya ukataji wa miti hovyo kwa ajili ya uchomaji wa mkaa pamoja na kuni.
Meneja wa kiwanda hicho, Mabeo Ngoelo, alisema mkaa huo mbadala unatengenezwa kwa takataka za makapi ya mpunga, magugu, mabua na zinazopatikana katika maeneo mbalimbali.
Mabeo alisema ujenzi wa kiwanda hicho ulianza Aprili 2, mwaka huu, ambapo awamu ya kwanza imegharimu kiasi cha Sh milioni 66.
Alisema taratibu za kumalizia ujenzi, kununua vifa, mashine, unaendelea na uzalishaji mkaa huo mbadala unatarajiwa kuanza Desemba, mwaka huu na kwamba utauzwa kwa bei nafuu.
Aidha, alisema kuwa pia kiwanda hicho kinategemea kuanzisha utengenezaji wa majiko banifu yatakayokuwa yanatumia mkaa kidogo.