F Migogoro ya ndoa yatajwa kuwa chanzo cha vitendo vya ukatili | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Migogoro ya ndoa yatajwa kuwa chanzo cha vitendo vya ukatili


Ongezeko la migogoro ya ndoa nchini imetajwa kuwa chanzo kikubwa cha vitendo vya ukatili na pia imesababisha watoto kukosa malezi ya wazazi wote wawili ambapo kwa mwaka kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Ustawi wa Jamii zinaonesha kwa muda wa miezi tisa kuanzia Julai, 2018 hadi Marchi 2019 jumla ya mashauri ya ndoa 16,832 yalipokelewa ukilinganisha na mashauri 13,382 kwa mwaka 2017/2018.


Hayo yamebainika leo jijini Dar es Salaam katika kikao katika ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wahariri wa vyombo vya habari katika kujengewa uelewa kuhusu Ajenda  ya  Kitaifa ya Wajibu wa  Wazazi /Walezi wa Malezi na Matunzo ya Familia.

Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi amesema kuwa vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kutoa elimu kwa jamii hivyo wana wajibu wa kuhakikisha wanatoe elimu itakayosaidia kujengeka kwa malezi bora kwa familia na watoto nchini.
Dkt. Ng’ondi  amesema vitendo vya ukatili vimezidi kukithiri nchini hivyo ameviomba vyombo vya habari nchini kuendeleza Ajenda hiyo ili kusaidiana na Serikali katika kupambana na vitendo hivyo.

Amesema kuwa kwa mujibu wa Utafiti wa hali ya ukatili dhidi ya watoto uliofanyika na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na UNICEF wa mwaka 2011 unaonesha kuwa mtoto 1 kati ya watoto 3 wa kike na 1 kati ya 7 wa kiume walifanyiwa vitendo vya ukatili kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Dkt. Ng’ondi ameongeza kuwa asilimia 72 ya wasichana na asilimia 71 ya wavulana walifanyiwa ukatili wa kimwili na vilevile robo ya watoto walifanyiwa ukatili wa kiakili.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Mwajuma Magwiza ameeleza kuwa wadau wote pamoja na wahariri na waandishi wa habari wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata malezi na makuzi bora kwa kuhakikisha wanajenga maadili na kiumairisha mila na desturi katika kujenga jamii iliyo bora.