Na John Walter-Babati
Mkuu wa wilaya ya Babati Eliz Elizabeth Kitundu ameungana na viongozi wa dini na wanasiasa katika futari aliyoiandaa mjini Babati.
Akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu na viongozi mbalimbali wa wilaya na Mkoa mkuu wa wilaya amewataka viongozi wa dini kuendelea kuitangaza vizuri serikali ya awamu ya tano kwa kuwa imefanya mambo makubwa.
"Serikali yetu mnaona inafanya maendeleo makubwa sana katika taifa letu,miradi mbalimbali inaendelea,barabara zimeboreshwa mijini na vijijini,huduma za afya,Elimu na maji' alisema Kitundu.
Amesema katika Halmashauri za Babati serikali imetoa fedha kwa ajili ya vituo vipya viwili vya afya huku ikisambaza dawa za kutosha katika hospitali na zahanati zote katika wilaya hiyo.
Aidha amesema miradi ya elimu inaendelea kutekelezwa ambapo maboma 46 Babati vijijini yanendelea kujengwa na kukarabatiwa huku shule zote za sekondari Babati mjini zikipatiwa fedha za kukamilisha ujenzi wa madarasa.
Mkuu wa wilaya amewashukuru viongozi wote ambao wamejitokeza na kusema kuwa imekuwa ni jambo la baraka kwake kwa kutoa mwaliko na viongozi hao kuonyesha moyo wa utayari.