Na Enock Magali, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, ametoa siku tano kwa Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. James Kiologwe kuhakikisha anapeleka wahudumu wa Afya katika Zahanati ya Soya Wilayani Chemba.
Dkt.Mahenge ametoa maelekezo hayo June 10 mwaka huu,wakati alipofanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kata hiyo ambapo awali wakitoa kero zao baadhi ya wananchi pamoja na kuzungumzia upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule yao ya msingi pia wamelalamikia suala la uhaba wa wahudumu wa Afya katika Zahanati yao.
"Mkuu wa Mkoa hapa kwetu Soya kuna wananchi wengi,tunaomba utuangalie suala la wahudumu,Dokta yupo lakini wahudumu wachache tunateseka sana kwa hilo"Alisema mmoja wa wananchi.
Na alipotakiwa kujibu juu ya changamoto hiyo,Mganga Mkuu Kiologwe amesema kuwa,kituo hicho kilikuwa na watumishi wanne na tayari wawili wamestaafu,hivyo kuahidi kupeleka watumishi wengine pindi watakapo patikana katika mwaka wa fedha.
"Hawa walipatikana baada ya watumishi wale 387 ambao mkoa ulipatiwa lakini nafikiri katika mwaka huu wa fedha pia tunaweza kupata watumishi wengine na tuseme tu endapo tutakapo pata tutahakikisha wanaletwa Chemba ili waweze kufika katika kituo hiki cha Soya"Alisema.
Kwa upande wake RC Mahenge yeye amemtaka Dkt.Kiologwe kuangalia sehemu nyingine yenye watumishi wengi na baadhi yao kuwahamishia katika kituo hicho.
"Hii kazi nakupa mpaka Jumamosi (June 15),uwe umeshapata waganga wawili au watatu wakuja hapa,angalia katika wilaya zote hakikisha unapata waganga kama kuna shida yoyote nishirikishe,kuna watu wengi sana hapa,RC Mahenge.
Katika ziara yake hiyo aliyoianzia wilayani Chemba pamoja na mambo mengine pia amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa Umwagiliaji,Ujenzi wa Darasa na Zahanati iliyojengwa katika kijiji cha Igunga