F RC Mtaka ampongeza Makamu Mkuu wa Chuo IFM | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

RC Mtaka ampongeza Makamu Mkuu wa Chuo IFM


Makamu Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Prof. Tadeo Satta  amewahakikisha wananchi wa Mkoa wa Simiyu na mikoa jirani kuwa ujenzi wa awali wa  tawi la Chuo hicho mkoani Simiyu, unatarajia kukamilika  Septemba mwaka huu na kuanza kudahili wanafunzi katika mwaka wa masomo 2019/2020 .

Profesa  Satta ameyasema hayo jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Tawi la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Simiyu katika kijiji cha Sapiwi wilaya ya Bariadi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amempongeza Makamu Mkuu wa Chuo IFM, Prof. Tadeo Satta kwa kuwa mtendaji wa mipango aliyoipanga na kutimiza ahadi ya kuanza kujenga tawi hilo mwaka huu, huku akitoa wito kwa  wananchi wote kuchangamkia  fursa mbalimbali ikiwemo ujenzi wa hosteli, migahawa na nyumba za kupangisha watumishi.

“Tawi la Chuo cha IFM linajengwa Sapiwi watu wote wanaalikwa kuchangamkia fursa na wachangamikiaji wa fursa wa kwanza ni wana Sapiwi wenyewe, tungehitaji kupata hosteli, migahawa ya chakula, maeneo ya watu kunywa vinywaji na tutawaambia TANROADS waone namna ya kuweka “stendi” maana hapa Sapiwi kitakuwa kituo kikubwa” alisisitiza Mtaka.

Aidha, Mtaka amewahakikishia viongozi wa Chuo cha IFM kuwa viongozi wa Mkoa wataendelea kushirikiana nao  katika kuhakikisha azma ya kukamilisha ujenzi kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuwezesha mkandarasi kufanya kazi saa 24 kwa kuhakikisha kuna ulinzi  na miundombinu ya umeme inakuwepo katika eneo la ujenzi.