Na Paschal D.Lucas,Mwanza
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa imeendesha mkutano wa wadau wa sekta ya mawasiliano Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kupokea maoni,mapendekezo na kusikiliza kero zinazohusu huduma za mawasiliano nchini.
Akizungumza wakati wa mkutano huo,Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo ameyataja baadhi ya majukumu yao kuwa ni kusimamia upatikanaji wa huduma zinazokidhi viwango na vigezo na masharti ya usambazaji wa bidhaa na huduma za mawasiliano,kudhibiti tozo na viwango vinavyohusiana na huduma za mawasiliano,kusimamia utendaji kazi wa sekta ya mawasiliano ukilinganisha na kiwango cha utekelezaji uliowekwa.
Mkutano huo wa siku moja umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza na kukutanisha wadau mbalimbali wakiwemo watoa maudhui kupitia TV,Radio,mitandao,mafundi simu,polisi,wauzaji na wasambazaji wa vifaa vya mawasiliano na wadau wengine Wa mawasiliano.