Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara hiyo ina mpango wa kuondokana na changamoto ya malisho ya mifugo ambayo imekuwa ikisababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Prof. Gabriel amesema hayo katika Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, kwenye hafla fupi ya kupokea matrekta saba kwa ajili ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) pamoja na Shamba la Malisho Vikuge kupitia mradi wa kuunganisha matrekta wa URSUS-TAMCO unaofadhiliwa na Serikali ya Poland.
Akizungumza katika hafla hiyo katibu mkuu huyo amesema matrekta manne ambayo yamenunuliwa na TALIRI kwa njia ya mkopo wa miaka miwili wenye thamani ya takribani Tshs. Mil 220 na matrekta matatu ambayo yamenunuliwa kwa fedha taslimu Tshs. Mil 192.1 na Ofisi ya Msajili Hazina kwa ajili ya Shamba la Malisho Vikuge, yatatumika kwa ajili ya kilimo kwenye mashamba ya malisho ya mifugo na kuongeza wingi wa upatikanaji wa malisho na yenye ubora kwa mifugo pamoja na kuondoa migogoro ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima pamoja na ufugaji wa kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho.