F Wawili mbaroni kwa kuvalia gwanda za JWTZ | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wawili mbaroni kwa kuvalia gwanda za JWTZ



Na James Timber, Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watuhumiwa wawili waliofahamika kwa majina ya Frank Ayubu (22), kabila Muha askari wa kujitolea Kambi ya JKT Ruvu na Khalifan Mohamed (20), Mnyamwezi Mkazi wa Kirumba wakiwa wamevalia sare zinazofanana na za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kitendo ambacho ni kosa la jinai.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Muliro Muliro ameeleza tukio limepatikana baada ya kupatikana kwa taarifa kwa intelejensia kwamba maeneo hayo wameonekana vijana waliovalia sare zinazofanana na sare za jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kamanda Muliro amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama walifanya ufuatiliaji wa haraka na kufika eneo la tukio na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa wamevalia sare hizo.

Muliro alisema kuwa polisi wapo katika mahojiano na watuhumiwa hao pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa shukrani za dhati kwa wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.

Pia Kamanda huyo alitoa onyo kwa baadhi ya vijana wenye tabia ya kupenda kuvaa sare zinazofanana na majeshi ya ulinzi na usalama wa Tanzania kuwa waache mara moja, kwani kufanya hivyo ni kosa na  wanaweza kujikuta wakiwa katika msuguano mkali na vyombo vinanavyosimamia sheria.