F Wizara ya Maji yatangaza kuanzisha wakala wa usambazaji wa maji vijijini | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wizara ya Maji yatangaza kuanzisha wakala wa usambazaji wa maji vijijini


Wizara ya Maji imetangaza kuanzisha wakala wa usambazaji wa maji na usafi wa mazingira vijijini ambapo wakala huu utakua na jukumu la kusimamia sekta ya maji vijijini ikiwemo kutekeleza usanifu, ujenzi na usimamizi wa miradi ya maji.


Akizungumza leo Jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Dk Kitila Mkumbo amesema wakala wa maji safi, usafi na mazingira vijijini (RUWASA) utaanza kutekeleza majukumu yake leo Julai 1, na utazinduliwa rasmi Julai 16, mwaka huu.

Amesema katika hatua za kukamilisha mchakato wa kuhamisha watumishi, mali na rasimali zingine zilizokua zikitumika na zilizokua idara ya maji katika mamlaka za Serikali za mitaa na Sekratarieti za Mikoa, kutakua na kipindi cha mpito cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu.

"Muundo wa RUWASA unajumuisha bodi ya wakurugenzi ya RUWASA, Menejimenti ya RUWASA makao makuu, Meneja RUWASA katika mikoa na wilaya. Tayari maafisa watakaokaimu nafasi mbalimbali za Uongozi wa RUWASA katika ngazi ya kitaifa na mikoa washateuliwa," Amesema Dk Kitila.

Katika hatua nyingine Wizara ya Maji imesema itakua na mkutano wa Saba wa mwaka wa Bodi za Maji na Mabonde kuanzia Julai 9-11, mwaka huu ambapo mwenyeji wa mkutano huo ni Bodi ya Maji ya Ziwa Tanganyika huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Maji, Prof Makame Mbarawa.

" Kauli mbiu ya mkutano huo ni Rasimali za Maji ni msingi wa Maendeleo Endelevu, Rasimali za maji zimeendelea kuwa kiungo muhimu katika nyanja nyingi za kiuchumi, kijamii kwa Maendeleo ya Dunia ya sasa na ijayo. Kwa hiyo ili kufikia mafanikio kazi ya uhifadhi wa vyanzo vya maji ni ya msingi na endelevu.