Na.Enock Magali Dodoma.
MKOA wa Dodoma umepokea rasmi Mwenge wa Uhuru 2019 unaotarajia kutembea umbali wa kilomita elfu 1,397 na kukagua miradi 47 yenye thamani ya shilingi bilioni 26.1.
Mwenge huo umepokelewa katika viwanja vya shule ya sekondari ya Pandambili wilayani Kongwa kutoka kwa kaimu katibu tawala wa mkoa wa Morogoro Noel Kazimoto kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Kebwe Stephen Kebwe.
Akipokea mwenge huo kwa niaba ya mkuu wa mkoa Dokta Binilith Mahenge, Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma Maduka Kessy amesema kati ya miradi inayotembelewa, miradi 19 itawekwa mawe ya msingi.
Aidha miradi 19 itazinduliwa na miradi 9 itatembelewa katika wilaya 7 na halmashauri 8 zilizopo mkoani humo ambapo kwa kuanza unaanzia wilaya ya Kongwa.
Maduka amesema kiasi cha fedha kinachogharamia miradi hiyo kimetoka kwa serikali shilingi bilioni 19.3, halmashauri shilingi bilioni 477.5, wafadhili shilingi bilioni 1.4 na wananchi shilingi bilioni 5.2.
Miradi hiyo inayotembelewa imekidhi kauli mbiu ya Mwenge 2019 isemayo maji ni haki ya kila mtu tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.
Katika mkoa wa Morogoro Mwenge wa Uhuru 2019 umetembea kilomita elfu 1,520 na kukagua miradi 48 yenye thamani ya shilingi bilioni 81.5 iliyopo kwenye wilaya 7 na halmashauri 9 zilizopo mkoani humo.