F Dodoma FC yaanza kwa kishindo ligi daraja la kwanza | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Dodoma FC yaanza kwa kishindo ligi daraja la kwanza



Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Timu ya Dodoma FC ya Dodoma imeanza  vyema mikikimikiki ya ligi daraja la kwanza kwa ushindi mnono baada ya kuifunga timu ya Cosmo politan bao mbili kwa bila, katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wakusisimua, ilikuwa dakika ya 36, Dodoma FC walipata bao la kwanza kupitia kwa beki wake mahili Mbwana Kibacha, kwa kuunganisha kwa kichwa mpira wa Kona uliopigwa na beki wa kushoto wa timu hiyo Hamad kibopile,na kuifanya timu hiyo kuwa mbele kwa bao moja kwa sifuri.

Hadi kipindi Cha kwanza kinamalizika Dodoma FC walikuwa mbele kwa bao moja kwa sifuri, kipindi Cha pili kilianza kwa kila timu kulisakama lango mpinzani wake,huku timu ya Cosmo politan wakionekana kumiliki Sana mpira hasa eneo la katikati, licha ya Mabadiliko ya hapa na pale kwa kila timu kuimarisha timu yake.

Walikuwa ni Dodoma FC tena walioandika bao la pili kwa mkwaju wa penati baada ya mchambuliaji wake Jamal Mtegeta kuangushwa kwenye eneo la hatari na mkwaju huo kufungwa na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Hamis Mcha, hadi mwisho wa mchezo Dodoma FC 2 na Cosmo politan 0.

Katika mchezo wa pili wa ligi hiyo Dodoma FC watakuwa nyumbani tena dhidi ya Friends rangers kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, wakati Cosmo politan watakuwa katika uwanja wa sabasaba mjini Njombe dhidi ya Njombe Mji.