F Kama kuna mtu anaamua kustaafu kwa hiari, hiyo ni haki yake - Rais wa TUCTA | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kama kuna mtu anaamua kustaafu kwa hiari, hiyo ni haki yake - Rais wa TUCTA


Na Amiri kilagalila-Njombe

Rais wa shirikisho la vyama vya wafanya kazi Tanzania TUCTA ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa Tanzania TALGWU bw.Tumaini Nyamhokya,amesema ni haki ya mfanyakazi kustaafu kwa hiari hivyo shirikisho halina tamko kwa wafanya kazi kutokana na habari zilizoenea mitandaoni kuwa watumishi wengi wameanza kuomba kustaafu kwa kuhofia KIKOKOTOO.

Rais wa TUCTA ameyasema hayo mkoani Njombe wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa Tanzania TALGWU mkoa wa Njombe ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili ukiambatana na uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

“Nimeulizwa na waandishi wa habari wengi kwamba watumishi wanastaafu kwa hiari wanakuwa na hofu,kustaafu kwa hiari kupo kwa mujibu wa sheria,mtu akiona atumie kustaafu kwa hiari ili apate fedha afanye mambo yake mengine hilo ni jambo jingine,na kama kuna mtu ameamua kustaafu kwa hiari ili asifike kule ambako kuna sintofahamu kwamba kuna KIKOKOTOO gani kitafuatia hiyo pia ni haki yake kwa mujibu wa sheria”alisema Nyamhokya

Nyamhokya ameongeza kuwa shirikisho hilo halina tamko la kuwaondoa hofu wafanyakazi.

“Kwa hiyo sisi hatuna tamko lolote la kuwaambia wafanyakazi,hatuna tamko lolote la kuwaondoa hofu,hofu ilikuwepo kubwa sana wakati kikokotoo kimebadilika na kikaja  kikokotoo ambacho kiukweli tunakiita kikokotoo kandamizi katika masalahi ya wafanyakazi hasa wale ambao wamekuwa wamestaafu sasa tumerejeshewa kiu na tumepewa muda wa miaka mitano tuweze kusimamia na kuandaa kwa hiyo timu zipo na zinaendelea kufanya kazi kuhakikisha tunaandaa kikokotoo ambacho kitakuwa rafiki kwa pande zote Mbili”aliongeza Nyamhokya

Katika hatua nyingine Nyamhokya amesema bado kuna badhi ya viongozi wa serikali na wanasiasa ambao wamekuwa wakifanya kazi za kimihemko na kuwaumiza watendaji hali ambayo inasababisha kuvunjika moyo kiutendaji.

“Sehemu kubwa viongozi wanakwenda vizuri lakini kuna baadhi ya wanasiasa ambao ni wateule wa mheshimiwa Rais, sisi kama viongozi wa vyama tunaona hawatendi vyema,baadhi tumeona wana hulka ya kuchukua hatua zinaonekana kuwa za kinidhamu kwenye majukwaa,utaona wanatamka simtaki mtumishi huyu mkoani kwangu,au wanasema kuanzia sasa wewe sio mkuu wa idara kiukweli inaumiza sana”alisema Nyamhokya

Katika taarifa iliyochapishwa hivi karibuni katika baadhi ya magazeti nchini ikiwemo  gazeti la mwananchi na baadhi ya mitandao ya kijamii inasema,wafanyakazi wa Serikali wafurika kuomba kustaafu kwa hiari.

Aidha inaongeza kuwa katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa taasisi ya Elimu ya juu,Sayansi,Technolojia,ufundi stadium,Habari na Utafiti, Winston Makere akizungumza katika semina ya viongozi wa RAAWU nchini jijini Arusha.

Idadi ya wafanyakazi ambao wanaomba kuacha kazi kwa hiari imeongezeka ili kulipwa mafao yao kabla ya 2023

Inasema Kumekuwapo na ongezeko kubwa la wafanyakazi wa Serikali, kuomba kustaafu kwa hiari ili kulipwa mafao kwa kikokotoo cha sasa ambacho kitafikia ukomo mwaka 2023.

Katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia Ufundi Stadi, Ushauri, habari na Utafiti (RAAWU) , Winston Makere  ametoa taarifa hiyo leo, Jumatatu Septemba 16 wakati anafungua semina ya viongozi wa RAAWU nchini kwa mujibu wa vyombo hivyo.

Amesema kutokana na ongezeko kubwa la watumishi kutaka kustaafu kwa hiari kabla ya miaka yao, hivi sasa wizara ya Utumishi, imeanza kusita kupokea maombi ya watu kustaafu kwa hiari.

"Ndio sababu bado tunaomba suala hili, tuendelee na majadiliano, awali tulipendekeza malipo ya mkopo yabaki asilimia 50 lakini Serikali ikapinga, tukapendekeza asilimia 40 pia ikakataliwa na sasa tunajadliana malipo ya asilimia 37.5,"amesema.

Mwisho wa kunukuu.