F Wabunge wa Jumuiya ya madola kanda ya Afrika waalaani vurugu zinazoendelea Afrika ya Kusini | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wabunge wa Jumuiya ya madola kanda ya Afrika waalaani vurugu zinazoendelea Afrika ya Kusini



Na Thabit Madai,Zanzibar.

Wabunge wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola kanda afrika wamelaani na kukemea vurugu za ubaguzi zinazoendelea Nchini afrika ya kusini hasa kwa wageni wanaotoka nje ya nchi hiyo.


Wabunge hao wasema kuwa vurugu hizo zimekuwa zinaleta athari kubwa ikiwemo uharibufu wa mali pamoja na mauaji kwa raia wageni.

Kauli hiyo walitoa wakati wakijadili hoja maalum juu ya vurugu hizo zinazoendelea nchini humo katika ukumbi wa hoteli ya Madinat Al Bahar Mbweni.


Walisema, imefika wakati kwa Afrika Kusini kutambua historia ya nchi yao katika kudai uhuru kwani nchi nyengine za Afrika zilichangia jambo hilo.

Mjumbe kutoka Ghana Sara Safu, alisema nchi hiyo watambue kuwa wahamiaji wanaotoka bara la Afrika sio maadui zao bali wanatumia uhuru wao wa kuishi wanapopataka.

“Imefika wakati sasa kuona CPA inachukua hatua kwani vurugu hizi sio mara ya kwanza kujitokeza zimekuwa zikijirejea mara kwa mara,” alisema.

Nae, Nancy Tembo kutoka nchini Malawi, alisema kuna umuhimu mkubwa wa kutolewa elimu kwa nchi hiyo na kutambua umuhimu wa nchi nyengine na historia zake.

“Sote tuna wahamiaji katika nchi zetu Malawi ina wahamiaji naamini na Tanzania pia ina wahamiaji lakini zipo njia za kisheria za kushughulikia watu hao sote ikiwa tutaendelea na tabia hii inaweza kuigwa katika nchi nyengine na hii ni hatari sana katika nchi zetu,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa, iwapo mtoto wako nyumbani anafanya vitendo vya utovu wa nidhamu kwa majirani basi fahamu kuwa nyumba yako itasemwa vibaya hivyo ni wajibu wa wazazi kuwafundisha watoto wao maadili mema kabla ya kupata sifa mbaya.

Mbunge kutoka nchini Kenya, John Mbadi, alisema kuendelea kwa vurugu hizo kwa wageni hupelekea visasi na chuki baina ya nchi na nchi na kurithisha vizazi vinavyokuja.   

Nae, Simai Mohammed Said kutoka Tanzania alisema ni vyema kuanzishwa kwa mitaala ya kufundisha uzalendo katika maskuli kwa watoto na kutambua historia ili kuwajenga vijana kufahamu umuhimu wa amani, utulivu na upendo kwa nchi ambazo walizisaidia.

Pia wabunge hao waliitaka CPA kutoa kauli kuhusiana na jambo hilo na kuweza kuchukuliwa hatua za haraka ili kukomesha jambo hilo.