F Halmashauri ya wilaya ya Njombe yatekeleza agizo la Rais Magufuli | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Halmashauri ya wilaya ya Njombe yatekeleza agizo la Rais Magufuli



Na Amiri kilagalila-Njombe

Halmashauri ya wilaya ya Njombe  mkaoani Njombe ambayo ni miongoni mwa halmashauri 31 ambazo zimepewa agizo na Rais Magufuli na kupewa mkazo na waziri wa ofisi ya Rais TAMISEMI Seleman Jafo kuhamishia ofisi zake maeneo ya uwatala, imefanikiwa kutekeleza agizo hilo kwa kupeleka ofisi zake katika kijiji cha Lunguya kata ya Mtwango wilayani humo.


Kabla ya kuhamishwa ofisi za halmashauri ya wilaya ya Njombe iliweka ofisi zake katika halmashauri ya mji wa Njombe hatua ambayo iliwafanya wakazi wengi wa vijijini ambako ndiko utawala wake uliko walikuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu wa zaidi km 30 hadi 55 kufata huduma za kiofisi mjini Njombe.

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa agizo hilo na jinsi utakavyo nufaisha wananchi wa wilaya ya Njombe Vijijini mkurugenzi wa halmashauri hiyo Ally Juma anasema hatua hiyo itapunguza gharama na kupoteza muda mwingi kusafiri huku pia akisema haitakuwa changamoto kubwa kwao kiutendaji katika makazi mapya kwa kuwa kijiji cha Lunguya kina huduma zote muhimu ikiwemo maji,umeme,barabara,na mawasiliano.

“Tarehe 26 tumeanza rasmi kuhamisha vifaa kama unavyoona  kwa magari yetu ya halmashauri,mali ya serikali tutahamisha kwa muda wa siku tatu kwa hiyo tarehe moja mwezi wa kumi na moja tutaanza kutoa huduma rasmi katika kata yetu ya Mtwango,wito wangu tu wakazi wa eneo hili la Mtwango wachangamkie fursa zilizopo kwasababu tunahama na watumishi karibu mia mbili wanakuja hapa”alisema Ally Juma

Kufuatia hatua hiyo nimezuru katika kijiji cha Lunguya kata ya Mtwango na kuzungumza na wakazi kuhusu ujio wa makao makuu ya halmashauri ya Njombe katika eneo lao wameshindwa kuzuia hisia zao kwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kutoa agizo hilo kwa kuwa awali ilikuwa kikwazo kikubwa kwao kufata huduma za kiutumishi zaidi ya km 40 mjini Njombe.


Azimio la kuhamishia makao makuu ya halmashauri katika kijiji cha Lunguya kata ya Mtwango liliazimiwa mara baada ya mvutano wa muda mrefu katika kikao cha baraza la dharura kilichoketi octoba 10 ambapo  mwenyekiti wa halmashauri Valentino Hongoli alitoa agizo kutangazia umma kuhusu eneo jipya la ofisi za halmashauri.