Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Timu ya Dodoma FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania bara, Leo imefanikiwa kutoka suluhu ya bila kufungana na timu ya Kagera Sugar ya Mkoani Kagera katika mchezo wa kirafiki uliopigwa katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Katika mchezo uliokuwa mkali na wakusisimua kwa dakika zote tisini kutokana na kila timu kucheza kiufundi zaidi na kutaka kupata bao la mapema, lakini mpaka dakika tisini zinamalizika hakuna timu iliyokuwa imepata bao.
Timu ya Dodoma FC huo unakuwa mchezo wa tatu kwa timu za ligi kuu, ambapo mchezo wa kwanza walicheza na Mbeya City na dhidi ya Singida United na leo dhidi ya Kagera Sugar na haijapoteza mchezo wowote mechi zote tatu.
Mara baada ya mchezo huo kocha wa Kagera Sugar Mecky Maxime amesema mchezo huo ulikuwa mahususi kwa ajili ya maandalizi ya michezo miwili ya Jijini Mbeya katika ligi kuu dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons na Dodoma FC kilikuwa kipimo sahihi kwao.
"Nashukuru mchezo umemalizika salama na timu wenyeji wametupa upinzani mkubwa, nadhani haya ni maandalizi mazuri kwetu katika michezo yetu miwili ya Jijini Mbeya dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons, na tunaamini tunaenda kushinda" amesema Maxime.
Nae kocha wa Dodoma FC Mbwana Makata amesema mchezo huo ni kwa ajili ya maandalizi kwa ajili ya ligi daraja la kwanza, na bado timu yake anaifanyia marekebisho hasa katika Safi ya ushambuliaji ili kuweza kupata mabao mengi.