Serikali imewataka Waajiri wote nchini kukitumia Chuo cha Watumishi wa Umma Tanzania katika kuwaendeleza Watumishi wao ili kuleta tija kiutendaji kwa lengo la kukuza na kuendeleza nchi yetu.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dr. Francis Michael katika mahafali ya 31 ya Chuo cha Utumishi wa Tanzania yaliyofanyika Kampasi ya Tanga.
Dkt. Francis amesema pamoja na umuhimu wa kukitumia Chuo cha Utumishi wa Umma kwa mafunzo, anahimiza waajiri kuwagharami watumishi wa taasisi wanazoziongoza ili waweze kushiriki mafunzo ya kuwaanda kufanya mitihani ya Utumishi wa Umma (Public Service Examination –PSE) ambayo ni mitihani ya lazima kwa watumishi wa umma wanaotakiwa kupanda vyeo.
Dkt. Francis ameupongeza uongozi wa Chuo kwa hatua mbalimbali zilizofanyika katika kuboresha Chuo hususani kwenye utoaji na usimamizi wa elimu ya vitendo kwa wahitimu wake yenye kuwajengea uwezo wa kiushindani katika soko la ajira, uimaarishaji wa mitaala kuendana na kasi ya mabadiliko ya sasa ya ukuaji wa uchumi wa viwanda, kuweka kituo cha Mafunzo kwa Watumishi wa Umma Makao Makuu ya Nchi Dodoma, Jengo la Maktaba Kampasi ya Tabora lililojengwa kwa mapato ya ndani na kutafuta maeneo katika kampasi ambazo zinatumia majengo ya kukodi.
Aidha, Dkt. Francis amewasihi wahitimu kutumia ujuzi na maarifa kama nyenzo muhimu katika kufanya kazi ili kuleta tija mahali pa kazi na kukuza uchumi wa Taifa.
Naye, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt Emmanuel S. Shindika kwa niaba ya Chuo amewapongeza wakufunzi wote kwa umahiri wao mkubwa katika kutoa huduma za mafunzo, tafiti na shauri za kitaaluma. Pia kuwashurukuru Taasisi mbalimbali za kiserikali na watu binafsi kwa misaada mbalimbali inayowezesha Chuo kusonga mbele.