Shirika la Ndege la SWISS International Airlines ambalo linamilikiwa na Shirika la ndege la Lufthansa la Ujerumani, limesimamisha safari za ndege zake zote aina ya Airbus A220 kutokana na matatizo ya injini zake.
Injini zote za ndege hizo zimelazimika kukaguliwa ili kuhakiki usalama wake. Ndege hizo hutumia injini aina ya PW 1500G zinazotengenezwa na kampuni ya Pratt & Whitney ya Canada.
Shirika hilo limesema lipo katika mazungumzo na mamlaka za usimamizi wa usafiri wa anga na pia mtengenezaji wa ndege hizo ambaye ni kampuni ya Airbus.
Mamlaka ya usafiri wa anga ya Marrekani FAA ilitoa muongozo kwamba injini zote za A220 ambazo ni Pratt & Whitney zinatakiwa kufanyiwa ukaguzi zaidi wa kiusalama.
Kusimamishwa kwa ndege hizo kunatokana na matatizo ya kiufundi ya mara kwa mara ya injini hizo. Mnamo July 25 vipande vya injini ya A220 vilikatikakatika na kuanguka katika anga la Paris, ndege hiyo ikiwa safarini kutokea Geneva kwenda London.
Tukio kama hilo linaripotiwa kutokea tena Septemba 16, kwa mujibu wa mamlaka ya uchunguzi ya ajali za ndege la Ufaransa, BEA. Na tukio lingine limetokea Octoba 15 likihusisha injini za P&W na kuwafanya marubani wa safari no LX359 kurudisha ndege Geneva na hatimaye shirika hilo kuamua kuzisimamisha ndege zake zote za A220.
SWISS ina jumla ya A220 zipatazo 29 amabapo 20 ni A220-300 na 9 ni A220-100. Safari zote za SWISS zilizopangwa katika ndege hizo zimeahirishwa.