Na John Walter-Hanang,Manyara.
Kukosekana kwa utaratibu mzuri wa kuielimisha jamii kutambua sheria za matumizi bora ya ardhi inatajwa kukwamisha juhudi za wawekezaji kufanya shughuli zao kwa ufanisi katika maeneo waliyowekeza hali inayosababisha migogoro isiyo ya lazima.
Katika Sheria za Ardhi Namba 4 na 5 za mwaka 1999,pamoja na mambo mengine inaeleza bayana madhara yatokanayo na Migogoro ya ardhi yanasababisha Uhasama, chuki na mgawanyiko miongoni mwa jamii ,Kupungua kwa uzalishaji mali na mazao ya chakula kutokana na kupoteza muda mwingi kwenye kutatua migogoro ya ardhi na kupotea kwa amani .
Mwekezaji wa shamba la Ngano Limited lililopo kijiji cha Gidagamowd Halmashauri ya wilaya ya Hanan'g mkoani Manyara Rilash Kalaiya, ameiomba serikali kumuimarishia ulinzi ili aweze kufanya uwekezaji wa tija bila kuathiriwa na wananchi wanaotoka mbali na kuvamia shamba lake.
Meneja huyo alisema wamejipanga vizuri kuwekeza ila wanakwamishwa na kukosekana kwa usalama wa uhakika kwa kuwa wamekuwa wakivamiwa na watu kutoka Karatu, Mbulu na Singida na kufanya uharibifu wa mitambo ya kufanyia shughuli za kilimo.
Aidha alisema changamoto nyingine katika uwekezaji wake ni uvamizi wa ng'ombe wa wanakijiji kwenye mashamba yake hali inayopelekea ardhi kuwa ngumu na kuharibu zana zinazotumika kulima na kupandia jambo linalowasababishia hasara kubwa.
Kalaiya amesema hao watu wanaovamia wanachochewa na baadhi ya wanasiasa wanaotafuta kura kupitia shamba hilo.
Hata hivyo ametoa ushauri kwa serikali kutoa elimu kwa wanakijiji juu ya namna ya kuheshimu uwekezaji ili naye awe kwenye mikono salama na afanye kazi kwa uhuru kwani yupo kisheria baada ya kupata ardhi hiyo kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania ambao wamempa Haki ya Matumizi ya ardhi anayoitumia.
Meneja huyo alisema shamba hilo alimilikishwa mwaka 2007 ambapo alipewa eka 42,000 ikiwa Gidagamowd anamiliki eka 15,000, shamba la Muljanda eka 12,000 na shamba la Serchet anamiliki ekari 15,000 na hivyo jumla ana ekari 42,000.
Alifafanua kuwa mpaka sasa ameshalima ekari 24,000 kati ya eka zote 42,000 za mashamba yake yote sawa na asilimia 76 huku akionesha kusikitishwa na wanasiasa wanaosema kuwa mashamba yake hajayaendelezwa.
Mwekezaji huyo ameiambia Muungwana Blog kuwa mwaka jana alivuna ngano gunia tatu na nusu kwa kila ekari kwenye kiasi gani Hekari 19 alizolima,na hiyo ni kutokana na hali mbaya ya hali ya hewa.
Ameeleza kuwa alifuata taratibu zote zinazohitajika katika kuwekeza, analipa kodi kwa mwezi shilingi Milioni saba hadi kumi kama inavyosisitiza serikali huku akidai kuwa makubaliano yao na Halmashauri ya wilaya ya Hanang ,ni kuboreshewa Miundo mbinu ya Bara ili aweze kufanya kazi zake kwa uhuru lakini hilo halijatimizwa ba na badala yake wao ndo wanamtaka ajenge barabara.
Makubaliano mengine anasema kuwa ni kutoa ajira, mahusiano mazuri na jamii, kutokodisha mashamba yao na kulima ngano.
Afisa kilimo wa shamba hilo Dismas Prones alisema wanafuata kanuni za kilimo ila changamoto waliyo nayo ni uvamizi .
Akimzungumzia Mwekezaji huyo Mkuu wa wilaya ya Hanan'g Joseph Mkirikiti, alisema Mwekezaji huyo amelima shamba lake kwa asilimia 26 tu na kuongeza kuwa, ofisi yake inaenda kulichukulia hatua suala hilo.”haiwezekani mwekezaji mpaka anaomba kujengewa barabara huyo hafai” alisema Mkirikiti.
Suala hilo pia liliibuka katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanan'g ambapo ambapo mwenyekiti wa Chama Cha mapinduzi(CCM) Mathew Darema aliibua hoja hiyo akitaka kunyang’anyw’a mashamba wawekezaji watatu ambao wanashindwa kuyaendeleza na kutotii makubaliano ya mambo ambayo walitakiwa kufanya.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hanan'g George Bajuta (CCM) alikiri kuwa yapo mashamba matatu ya wawekezaji ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza na kuyataja kuwa ni shamba la Sechent, shamba la Gidagamowd na Murunjanda.