F RC Makonda atoa tena eneo la Barabara ya chuo cha IFM kwa wachonga vinyago, wachoraji na wauza shanga | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

RC Makonda atoa tena eneo la Barabara ya chuo cha IFM kwa wachonga vinyago, wachoraji na wauza shanga

Kufuatia ugeni Mkubwa wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka Nchi 29 za Afrika na Nchi 5 Nordic wanaotaraji kuingia nchini kuanzia kesho kwaajili ya mkutano, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda ameamua kutumia fursa ya mkutano huo kuwapatia Ulaji Wachonga Vinyago, Wachoraji na wauzaji wa shanga kwa kuwakabidhi eneo la Barabara ya Chuo cha IFM posta ili waweze kuuza na kutangaza bidhaa zao kwa wageni hao wanokuja kwenye mkutano huo.

RC Makonda amesema Mkutano huo unatarajia kufanyika November 08 na utafunguliwa na Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC.)

Aidha RC Makonda amezitaja Nchi 5 za Nordic zitakazoshiriki Mkutano huo kuwa ni Sweden, Norway, Denmark, Finland na Iceland ambapo kwa Upande wa Afrika Nchi zitakazoshiriki ni Algeria, Angola, Benini, Botswana, Burkina Faso, Burundi, Comoro, Kongo DRC, Misri, Ethiopia, Ghana, Kenya, Lesotho, Mali, Malawi, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria,Niger, Rwanda, Senegal, Somalia, Afrika Kusini, Tunisia, Uganda, Zambia, Zimbabwe, na Wenyeji Tanzania.

Pamoja na hayo RC Makonda amesema anaamini kwa siku nne alizowapatia Wafanyabiashara hao wataonyesha na kuuza bidhaa zao jambo litakalosaidia pia kutangaza utalii wa Tanzania kwakuwa Licha ya ujio wa Mawaziri hao pia wataambatana na Mabalozi wa Nchi hizo.

Katika hatua nyingine RC Makonda amewaomba wamiliki wa Mall zote kuongeza muda wa kutoa huduma hadi usiku ili kutoa nafasi kwa Wageni kufanya Manunuzi ya vitu mbalimbali.

Hata hivyo RC Makonda amewataka wachonga Vinyago, Wachora picha na Watengeneza Shanga kuja na mkakati endelevu wa kuhakikisha angalau kila baada ya miezi miwili au mitatu wanapewa eneo katikati ya mji kwajili ya kuuza na kutangaza bidhaa zao.